Na Mwandishi Wetu.
MASHINDANO ya mbio fupi za magari ya Sao Hill Misitu Auto Cross ambayo yamefanyika kwa mara kwanza katika Shamba la Miti Sao Hill lililopo wilayani Mufindi mkoani Iringa yamefana kwa kiwango kikubwa huku washiriki wa mashindano hayo wakiomba mashindano hayo yafanyike kila mwaka pamoja na kuandaliwa mashindano makubwa ya Bara la Afrika.
Akizungumza baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mashindano hayo katika Shamba la Miti Sao Hill linalomikiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo Lucas Sabida amesema ndio mara ya kwanza kwa Wakala huo kuandaa mashindano hayo ikiwa ni utalii mpya ambao wameutambulisha kwenye sekta ya utalii nchini.
“Katika shamba la Sao Hill fursa ziko nyingi , tunazalisha bidhaa zinatokana na mbao , asali na tunazo fursa za uwekezaji .Lakini sasa tumekuja na utalii wa michezo kwenye maeneo yetu ya hifadhi za misitu ya asili na ile misitu ya kupanda kama Sao Hill kama ambavyo leo tumeanza na mbio fupi za magari.
“Sao Hili tunalo eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 155,000 na zina barabara zenye urefu wa kilometa 1,500 kwa hiyo ukiunganisha hizi barabara unaweza kutoka hapa(Sao Hill) hadi Mwanza .Hivyo tunaweza kufanya mashindano makubwa ya ya magari hata ya Bara la Afrika,”amesema.
Ameongeza katika shamba la Miti Sao Hill inawezekana kufanyika michezo ya aina yoyote kwani kuna eneo kubwa na la kutosha lakini TFS wameamua kuanza na mashindano ya magari ambayo wanatarajia yatakuwa yakifanyika kila mwaka kwa kushirikiana na wadau wengine.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule mkoani Iringa amesema utalii wa mashindano ya mbio za magari kwenye Shamba la Sao Hill unakwenda kufungua fursa zaidi katika sekta ya utalii na wao wamejiandaa kupokea wananchi na wawekezaji walio tayari kufanya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.
Amesema sekta hiyo imeendelea kukua kwa kasi kubwa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipotangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuanzisha filamu ya Tanzania Royal Tour na sisi kupitia sekta ya misitu tumeona pamoja na kupata mbao na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu tunaamini mashindano ya magari yataongeza fursa na kuleta bidhaa mpya kwenye sekta ya misitu .
“Pia tunawapongeza TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ikiongoza na Balozi Pindi Chana kwa uratibu mzuri wa mashindano haya ya magari yanayofanyika hapa. Kwetu mashindano haya ya magari yanakwenda kuongeza fursa nyingine kwa wananchi wetu,”amesema.
Wakati huo huo Ofisa wa TFS Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji Utalii Ikolojia Anna Lawuo amesema TFS imeamua kulitumia shamba la Sao Hill kwa ajili ya kufanya mashindano hayo mafupi ya mbio za magari na kwamba mashamba yao yamepangiliwa vizuri kwani kuna barabara zinazopitika na zenye vikwazo.
“Kwa hiyo leo tuko hapa kwa ajili ya maonesho ya mashindano ya magari ya majaribio lakini ni katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za utalii maana yake yeye alianzisha Royal Tour ambayo imeleta watu ,wawekezaji lakini hiyo Royal Tour iweze kuleta maana zaidi ni vizuri tukaunga mkono kwa kuja na vitu vingine vya ziada,
“Leo tumefanya kitu tofauti kabisa ambacho kwanza hakijawahi kufanya kwenye misitu ya hifadhi na hata Sao hill , hivyo TFS tumeamua kuanzisha mashindano ndani ya Sao Hill na yamekuwa na muamko kubwa.Tuna mpango wa kuandaa mashindano makubwa yatakayoitwa Afrika Chapionship Rally na yatafanyika hapa Sao Hill,”amesema
Kwa upande wa Mchezeshaji wa Mbio hizo za magari John Makeo amesema mashindano hayo yamefanyika ya kilometa sita na kila mzunguko ulikuwa ni kilometa 1.5.“Mbio fupi lengo lake ni kuwaanda madereva wa kesho na keshokutwa , kikatiba mbio hizo zinatakiwa kuchezwa kilometa moja, isizidi kilometa 1.5.”
Aidha amesema Sao Hill kuna maeneo mazuri kwa ajili ya kufanya mashindano ya mbio za magari hasa kwa kuzingatia kuna eneo la kutosha na bahati nzuri hakuna makazi ya watu zaidi ya msitu ulitokana na miti ya kupandwa na miti asili.
Toa Maoni Yako:
0 comments: