Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) akiongoza Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, Kamisheni ya Bonde la mto Songwe uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi ambapo masuala ya rasilimali za maji yanayozihusu nchi za Tanzania na Malawi yamefanyiwa kazi kwa ushirikiano na wataalamu wa pande zote mbili za nchi hizo. Kushoto ni Waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Malawi Mhe. Abida Sidik Mia (Mb).
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) akipitia makabrasha kuhusu Mkutano Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, Kamisheni ya Bonde la mto Songwe Jijini Lilongwe. Wizara ya Ardhi ni moja ya wizara muhimu katika kufanikisha kazi mbalimbali za maendeleo ya wananchi katika bonde hilo.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, Kamisheni ya Bonde la mto Songwe uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi. Katikati ni Dkt. George Lugomela, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Tanzania.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) pamoja na Waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Malawi Mhe. Abida Sidik Mia (Mb) wakisaini makubaliano ya kuendesha vikao vya Mawaziri vinavyohusu Kamisheni ya Bonde la mto Songwe, tukio limefanyika Lilongwe nchini Malawi.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Tanzania inaendelea kunufaika pamoja na wananchi wake kwa kujenga uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali, zikiwemo nchi jirani zinazoizunguka.

Mhe. Mahundi amesema hayo wakati wa Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.

Amesema kupitia Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe kazi inafanyika kwa ushirikiano kuondosha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Tanzania na Malawi kupitia wataalamu wa rasilimali za maji, ikiwemo ujenzi wa mabwawa katika bonde hilo ambayo itakuwa suluhu ya mafuriko yanayoharibu mali mbalimbali ikiwamo mazao kwa kujenga bwawa la Songwe Chini, na mazingira.

Aidha, kuwezesha kilimo cha umwagiliaji zaidi ya hekta 6,000 na kupata nishati ya uhakika ya umeme kwa nchi mbili kugawana megawati zipatazo 180.

Mhe. Mahundi amesema hayo ni mafanikio ya mahusiano yaliyojengwa na viongozi wa nchi mbili katika kuhakikisha wananchi wanafanya kazi kwa maendeleo ya nchi zao.

Amesema kazi hiyo ni matunda ya viongozi Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Lazarus Chakwera , Rais wa Malawi.

Pamoja na hatua hiyo, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha huduma ya maji na miradi ya maji inakuwa endelevu na kutosheleza mahitaji ya jamii kwa sasa na vizazi vijavyo.

Kamisheni ya Bonde la mto Songwe inaundwa kwa Pamoja na nchi za Malawi na Tanzania, ambapo katika kikao hicho Mawaziri wamekubaliana na kusaini Kanuni za uendeshaji wa vikao vya Mawaziri.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: