MENEJA wa Ulinzi na Mshirika Katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama Vodacom PLC Makao Makuu, James Wawenje amepanda kizimbani leo Jumatano, Oktoba 20, 2021 kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya Hai, Lengai ole Sabaya na wenzake sita.
Shahidi huyo wa sita wa Jamuhuri akitoa ushahi wake mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Arusha, Patricia Kisinda amesema idara yake ndiyo inahusika na mfumo wa kunakili kumbukumbu za kupiga na kupokea simu na kunakili ujumbe wa simu.
Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Ofmed Mtenga amesema idara yake pia ndiyo inahusika na kunakili kumbukumbu za kutuma na kupokea miamala.
Amesema amekuwa mwajiriwa wa Vodacom tangu Agosti 25, 2015 na ana shahada uzamili masuala ya utawala katika ulinzi aliyoipata nchini Uingereza. Amesema katika majukumu yake wateja wake wakubwa ni Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mahakama na taasisi zingine kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato (TRA) na tume za ushindani.
Wawenje ameileza mahakama kuwa amekuwa akishirikiana kutoa taarifa za uchunguzi kwa mujibu wa sheria. Kusimamia ulinzi na mali za kampuni na kishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa nyaraka zinapohitajika kwa mujibu wa sheria. Katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27, 2021 washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano la kwanza ambalo ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh90 milioni huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.
Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai. Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili Moses Mahuna, Fauzia Mustapha, Edmund Ngemela na Fridolin Gwemelo.
Katika shauri hilo Jamuhuri inawakilishwa na wakili mwandamizi Ofmed mtenga na Felix Kwitukia na Wakili Neema Mbwana. Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments: