Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Sekta ya Habari na Utangazaji ni moja ya sekta inayotoa huduma kwa jamii ya watu wengi nchini ambayo ni haki ya msingi ya raia kama inavyoonekana kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha kutoa na kupokea habari kunatambuliwa duniani kote kuwa ni moja ya haki za binadamu ambapo Umoja wa Mataifa, na umoja wa afrika zina matamko rasmi ambayo Serikali imeridhia kuhusu haki ya kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote. haki hii kama zilivyo haki nyingine zote, hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii na uhuru binafsi wa binadamu

Mei 3 kila mwaka Tanzania pamoja na nchi nyingine Ulimwenguni huadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari tangu Umoja wa Mataifa ulipoidhinisha siku hiyo ikiwa na lengo la kuwapatia watu taarifa na elimu za kujenga demokrasia na maendeleo katika sekta ya habari

mwaka huu 2021 kilele cha maadhimisho haya nchini Tanzania yamefanyika Jijini Arusha na kujumuisha washiriki kutoka sekta ya habari inayojumuisha Serikali kupitia Idara ya Habari MAELEZO, vyombo vya habari binafsi na vya Serikali, Mashirika ya Kimataifa, wadau wa maendeleo na asasi zisizo za kiserikali na wadau wengine mbalimbali wameshiriki kwa kufanya midahalo mikubwa pamoja na waandishi wa habari kutembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kutangaza vivutio vyetu na kuutangaza urithi wa dunia na kwa madhumuni ya kuvutia watalii.

mwaka huu maadhimisho haya yamekuja na kauli mbiu ya "Habari kwa Manufaa ya Umma" ambayo inasaidia kujua namna ambavyo habari zinamanufaa kwa umma,ikiwemo haki ya kikatiba ya kupata habari na kwa mwaka huu Jamhuri ya muungano wa tanzania katika siku ya uhuru wa vyombo vya habari imejikita katika maeneo makuu matano ya vipaumbele ambavyo ni Uhuru wa vyombo vya habari vinavyofaa, kuendeleza nguvu kazi, mazingira mazuri ya sheria na sera, ikiwa ni pamoja na hali bora ya kazi, ulinzi na usalama wa waandishi na kujua kufanya kazi za kiuandishi, ikiwa ni pamoja na uelewa wa matumizi ya kidijitali

katika kuhakikisha habari zinanufaisha umma Serikali imedhamiria kuweka mifumo ndani ya vyombo vya habari inayowalazimisha kuleta matokeo chanya hasa ya matumizi ya sheria hususani kwa wahariri na watekeleza sera kama Maafisa Utumishi, ikiwa ni sambamba na kupitia upya sera ya vyombo vya habari ya mwaka 2003.

katika hotuba iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alisema kuwa, Serikali itaboresha mazingira katika sekta ya habari ili Waandishi wa Habari watekeleze majukumu yao bila hofu, na kwa kujiamini.

"Serikali itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili muweze kutekeleza majukumu yenu bila hofu, na kwa kujiamini huku mkizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo yao,"amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa alisema ili kuweza kuendana na lengo namba 16 la Maendeleo Endelevu (SDG16), Tanzania itahitaji kuwa na ukusanyaji wa fedha wenye tija na wa kudumu, takwimu zenye ubora zinazozalishwa na kushirikishwa kwa umma, ambapo matokeo yake yanaweza kufanyiwa majaribio na kupimwa maendeleo yake.

"Ni muhimu kuwa na mpango wa maendeleo ili kuviwezeshe vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Waandishi wa Habari wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo za matunzo, na mishahara midogo kwa wafanyakazi, mapato yasiyotosheleza, na kukosa kinga bima ya afya kwa waandishi pamoja na wasaidizi wao. Mambo haya yamekuwa ni tatizo na kuleta wasiwasi kwa wanahabari," amesema Bashungwa.

Aliendelea kueleza kuwa, Serikali inahimiza wadau wote wa habari, kuhakikisha wanaweka utaratibu utakaowezesha kufanya ufuatiliaji, na uwajibikaji katika kutekeleza sera na sheria za nchi, pamoja na miongozo kwa umma na jamii kwa ujumla. Miongozo hiyo izingatie kuwepo kwa mazingira na hali bora ya kazi, ulinzi na usalama wa waandishi, kujua kufanya kazi za kiuandishi, ikiwa ni pamoja na uelewa wa matumizi ya kijiditali.

"Serikali ya awamu ya sita inathamini na kutambua uhuru wa vyombo vya habari na katika muktadha huo hivi karibuni Serikali ilivifungulia vyombo vya habari vya kielektroniki vya online TV vilivyokuwa vimefungiwa kwa makosa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vinafanya kazi kwa uhuru na kukuza ajira za vijana nchini,"amesema Bashungwa.

katika kuonesha uhuru wa vyombo vya habari nchini, Waziri Bashungwa alieleza kua Tanzania ni miongozi mwa nchi chache zenye vyombo vingi vya habari Barani Afrika ambapo mpaka sasa kuna jumla ya Magazeti 246, Televisheni 53, Redio 194, Redio za Mtandaoni (Online Radio) 23, Blogs 120 na Televishenio Mtandao (Online TV) 440. ambapo ishara kuwa nchi yetu inathamini na kuenzi vyombo na taaluma ya habari, na kusema Serikali iko tayari kushirikiana kuhakikisha na kunakuwepo na uwazi katika upatikanaji wa habari kwa Watoa Huduma ya Mitandao, kama sehemu muhimu ya habari kwa manufaa ya umma.

“Ni vyema mkatambua kuwa jukumu lenu kubwa kama washiriki katika mjadala huu ni kuhakikisha kuwa mapendekezo mtakayotoa yataleta mafanikio. Mafanikio hayo yatapatikana iwapo wadau wote tutashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo na maazimio. Kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Sita (06) inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, tunawahakikishia ushirikiano mkubwa.” Amesema Bashungwa

Pia Waziri ametoa wito kwa Viongozi mbalimbali ndani ya Serikali kuhakikisha anaondoa vikwazo na kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanapohitaji taarifa muhimu kwa Manufaa ya Umma na maslahi ya Taifa letu kwa ujumla.

Kuhusu changamoto Waziri Bashungwa amesema anazitambua changamoto nyingi zinazowakumba aandishi wa habari wakati wa kutekeleza majukumu ya kila siku, zikiwemo kunyimwa taarifa bila sababu ya msingi hata kama mwandishi anakuwa na kitambulisho kilichotolewa na Serikali kumtambulisha kama ni mwandishi wa habari. na kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan inazitambua changamoto hizo na itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili kuwawezesha kutekeleza majukumu ya kiuandishi bila hofu, na kwa kujiamini na kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Taifa.

sambamba na hilo, waziri bashunga ametoa pongezi nyingi kwa Shirika la Umoja amataifa , elimu sayansi na utamaduni (UNESCO) kwa kuendelea kuiunga mkono na kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuendeleza uchumi a nchi yetu na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo"kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano a Tanzania, ninapenda kuwapongeza na kuwashukuru UNESCO ka kushirikiana na Serikali katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu. niwapongeze kwa kusaidia kufanikisha maadhimisho haya, tangu mwanzo hadi mwisho. UNESCO mmekuwa mkiipatia Tanzania misaada ya kiufundi, kwa zaidi ya miaka arobaini na saba (47) sasa. Hivyo sisi kama serikali, hatuna budi kuapongeza, na kuaahidi ushirikiano mkubwa kutoka kwetu" amesema Bashungwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: