MBUNGE wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina ameshauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikaangalie kwa kina hoja zote zilizoibuliwa kwenye taarifa ya CAG na kuhakikisha watuhumiwa wote wamejumuishwa katika hatua ya kutoa adhabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake ambazo ni Sheria za Fedha, Bajeti na Manunuzi.

Akizungumza jijini Dodoma, Mpina ameshauri hoja zote zilizowasilishwa na CAG baada ya uchambuzi wa Kamati ya PAC na LAAC ziandaliwe kwenye bangokitita itakayoonesha hoja ilivyoletwa na uhalisia baada ya uchambuzi wa kamati hizo ili ukweli ujulikane.

Mpina amesema kwa mujibu wa taarifa ya CAG inasema usimamizi usioridhisha wa Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii kuanzia mwaka 2019/20 na 2017/2018 bilioni 34.9
Imesema kiasi cha fedha sh. bilioni 5.4, sh. bilioni 2.8 na sh. milioni 100 zilihamishwa na Mkurugenzi wa Utalii kwenda Bodi ya Utalii, Chuo cha Taifa cha Utalii na Makumbusho ya Taifa bila idhini ya Afisa Masuuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mpina amesema ripoti hiyo inasema kiasi cha sh. bilioni 6.9 zililipwa toka kwenye Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii bila idhini ya Afisa Masuuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kiasi cha sh. bilioni 16.36 zililipwa bila ya kuwa na hati za malipo na bilioni 11.156 zilikuwa na upungufu wa nyaraka na kwamba Malipo ya namna hiyo ni kinyume na Kanuni ya 88 (1) za fedha za mwaka 2001 na Kanuni ya 9 (2) na 11 ya Kanuni za Tozo ya Maendeleo ya Utalii ya mwaka 2013.

Mpina anasema hata hivyo CAG anapendekeza Mkurugenzi wa Utalii na Mhasibu ndio wanahusika na usimamizi mbaya wa fedha za tozo la Mfuko wa Maendeleo huku akimuondoa Katibu Mkuu wizara hiyo kwenye tuhuma hizo.

Mpina amejiuliza fedha zilitokaje bila idhini ya Afisa Masuuli?, Miaka miwili ya fedha mfululizo fedha zilitoka kwenye mfuko wa maendeleo ya utalii bila afisa masuuli kujua? Kama ndivyo nafasi yake ya usimamizi iko wapi.

Serikali imeboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi kwa kutumia njia ya TEHAMA inawezekanaje fedha zote hizo zikatoka bila kuidhinishwa na mamlaka husika?

“Shida yangu hapa ni kwa nini wahusika wengine wanalindwa na kukikingiwa kifua na taarifa ya CAG kinyume na Sheria ambazo amezinukuu yeye mwenyewe ilihali watuhumiwa hao wanafahamika ili kukuza dhana ya uwajibikaji kwa wote” anauliza Mpina

Hivyo Mhe. Mpina ameshauri Kamati ya PAC ikaangalie kwa kina hoja hiyo na kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wamejumuishwa katika hatua ya kutoa adhabu.

Pia Hoja zote zilizowasilishwa na CAG baada ya uchambuzi wa Kamati ya PAC na LAAC ziandaliwe kwenye matrix itakayoonesha hoja ilivyoletwa na uhalisia baada ya uchambuzi.

Pia Mpina ameibua hoja nyingine inayohusiana na Maliasili na Utalii ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), zilifadhili Tamasha la upandaji Mlima Kilimanjaro bila kuidhinishwa katika bajeti kiasi cha sh. Milioni 171.9.

Pia TANAPA ililipa Kampuni ya Asante Tours and Safari’s sh. Milioni 57.4 kwa ajili ya gharama za malazi kwa wapandaji mlima ambapo ilibainika kuwa kazi ilipatikana bila ushindani na hapakuwepo na mkataba Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii iligharamiwa na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kiasi cha sh. Milioni 148.2 bila fedha hizo kuwepo kwenye bajeti.

Mapendekezo ya CAG hatua zichukuliwe kwa Waziri na Katibu wa Waziri huku akiwaacha Maafisa Masuuli wote ambao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Watendaji Wakuu (CEO’s) wa TANAPA, NCAA na TFS.

Mpina amejiuliza kwanini Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya TANAPA, NCAA na TFS wamekingiwa kifua na ripoti ya CAG.

Pia anayetangaza Zabuni na kuingia mikataba sio Waziri bali ni maafisa masuuli kwanini adhabu ielekezwe kwa Waziri pekee. Fedha huidhinishwa kutumika na maafisa masuuli na ndio wasimamizi wakuu wa bajeti kwanini makosa yaelekezwe kwa Waziri peke yake.

Hivyo ameshauri Kamati ya PAC ikaangalie kwa kina hoja hii na kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wamejumuishwa katika hatua ya kutoa adhabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake ambazo ni Sheria za Fedha, Bajeti na Manunuzi.
Pia Hoja zote zilizowasilishwa na CAG baada ya uchambuzi wa Kamati ya PAC na LAAC ziandaliwe kwenye bangokitita itakayoonesha hoja ilivyoletwa na uhalisia baada ya uchambuzi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: