Wadau wa Kilimo kutoka sekta binafsi, sekta ya umma (Wizara, Idara na Wakala), taasisi zisizo za kiserikali na washirika wa maendeleo kutoka ngazi ya kitaifa na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Kongani ya Mbarali) watakutana Vwawa wilayani Mbozi kwenye mkutano wa siku mbili tarehe 24 na 25 November, 2020 kujadili njia bora za ushirikiano ili kuboresha na kuendeleza kilimo cha kimageuzi.
`Mkutano huo umeandaliwa na Kituo cha kukuza kilimo ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT Centre Ltd) kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kituo cha SAGCOT Pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe, mkutano huo utatoa jukwaa la mazungumzo kati ya wadau juu ya maswala muhimu kwa ukuaji wa sekta ya kilimo katika Kongani ya Mbarali.
Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na kilimo endelevu kinachozingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira, masuala ya udhibiti na sera; fursa mpya za uwekezaji katika uzalishaji, usindikaji na uuzaji na vile vile kukubaliana juu ya njia za kutambua fursa hizo au kubuni njia za kutatua changamoto mbalimbali.
Mkutano huo utatoa jukwaa la kujadili vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo katika Kongani ya Mbarali na kupendekeza njia bora za kuboresha biashara ya kilimo. Sekta ya umma inatarajiwa kueleza majukumu yake mbalimbali ya uratibu wa shughuli mbalimbali za kilimo katika maeneo husika huku sekta binafsi ikipata fursa ya kueleza mbinu mbalimbali za ubunifu mpya, maendeleo na changamoto zinazowakabili katika minyororo mbalimbali ya thamani.
Miradi mbalimbali ya washirika wa maendeleo inatarajiwa kutoa taarifa za maendeleo ya miradi hiyo zinazoendelea na zilizopangwa kufanyika kwenye Kongani ya Mbarali. Asasi za Kiserikali zitawasilisha kuhusu majukumu ya uwezeshaji yanayotekelezwa na mashirika yao katika kuboresha uzalishaji wa kilimo na tija, maswala ya kijamii na mazingira pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo.
Mkutano huo pia utatoa fursa ya kipekee kwa wahusika kuchukua majukumu maalum na kuazimia juu ya utekelezaji kwa kutia saini taarifa thabiti ambayo itasainiwa na Sekta ya Umma, Sekta Binafsi pamoja na wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa wanaofanya kazi katika Kongani ya Mbarali na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo, maendeleo ya biashara, huduma za ugani na mashirika ya utunzaji na uhifadhi mazingira.
Akizungumzia Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, amesema ni fursa ya kipekee kwa wadau wa kilimo kujadiliana na kuweka misingi thabiti ya kuboresha sekta ya kilimo.
“Kilimo endelevu chenye tija na kichozingatia ujumuishi na utunzaji na uhifadhi wa mazingira mkoani Songwe kinawezekana katika kukuza uchumi wa viwanda”.
Toa Maoni Yako:
0 comments: