Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya Shirika hilo kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam leo Disemba 12, 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akifafanua jambo katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mafanikio ya Shirika hilo kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam leo Disemba 12, 2019.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanya mageuzi makubwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kadogosa alisema kuwa pamoja na mageuzi yanayoendelea katika sekta mbalimbali hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kufufua miundombinu ya reli katika maeneo mbalimbali ikiwemo njia ya treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Kilimanjaro ambayo kwa sasa inasafiri mara tano kwa wiki.
“Kutokana na maombi ya wananchi wengi tumeamua kwamba kuanzia Desemba 16 mwaka huu safari ya treni kutoka Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro itakuwa ni mara tano kwa wiki” alisema Kadogosa.
Kadogosa alieleza kuwa TRC imefanikiwa kuongeza idadi ya mizigo ambapo zaidi ya tani 1,456,537 zimeweza kusafirishwa katika reli ya kati (Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma) na kwa upande wa abiria treni za mikoani wameongezeka kutoka 411,172 mwaka 2014/15 hadi 578,439 mwaka 2018/19.
Sambamba na hilo, TRC imeweza kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 17.4 mwaka 2014/15 hadi bilioni 30 mwaka 2018/19 kwa treni za mizigo, kutoka bilioni 8.3 hadi bilioni 10.7 kwa treni za abiria wa mikoani na kutoka milioni 316.6 hadi bilioni 1.96 kwa treni za mjini.
Aidha TRC inajivunia mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali katika sekta ya reli kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) wenye gharama ya shilingi trilioni 7.5
“Mradi wa SGR katika mindombinu ya reli hapa nchini ni mradi mkubwa sana ambao utamwezesha mfanyabiashara au abiria wa kawaida kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi mwanza kwa saa 9 na treni hii itakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 160 kwa saa hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi hapa Tanzania” alieleza Kadogosa.
Alisema kuwa mpaka sasa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa (SGR) yenye mtandao usiopungua kilometa 2,561 umefikia asilimia 70 ambapo reli hiyo itaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na Katavi pamoja na nchi zisizokuwa na bandari (Rwanda, Burundi na DRC Congo).
Pia Kadogosa aliongeza kuwa TRC inatekeleza mradi wa uboreshaji wa reli ya kati- TIRP wenye lengo la kuongeza ubora na uimara wa njia ya reli kutoka Dar hadi Isaka ili kuweza kubeba mizigo kufikia tani 18.5 na mwendokasi wa kilometa 70 kwa saa.
Mradi huo wa TIRP umezalisha ajira kwa vijana wa kitanzania zaidi ya 1,600 pamoja na kuwanufaisha wafanyabiashara mbalimbali na watoa huduma.
Toa Maoni Yako:
0 comments: