Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Amassu Tadesse (kushoto), alipotua katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma akiwa katika ziara yake ya kikazi hapa nchini. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Doto James.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Admassu Tadesse (hayupo pichani) kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, jijini Dodoma. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiteta jambo na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Admassu Tadesse, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Rais huyo na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli. 
Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Dkt. Admassu Tadesse (kulia) akimweleza jambo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) walipokutana na kufanya mazungumzo, Jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua wakisikiliza kwa makini mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango (Mb) na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Dkt. Admassu Tadesse (hawapo pichani), Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Dkt. Admassu Tadesse (kulia), wakifurahia jambo baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Tanzania na Benki hiyo walipokutana Jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika ulioongozwa na Rais wa Benki hiyo Dkt. Admassu Tadesse (wa nne kulia) jijini Dodoma.Picha na Josephine Majura WFM – DODOMA).
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kushoto) akiongoza ujumbe wa Tanzania kumpokea Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Dkt. Admassu Tadesse alipowasili Uwanja wa Ndege Jijini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, Dodoma.

RAIS wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Admassu Tadesse ameahidi kuwa Benki yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuipatia mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi yake ya kimkakati ya maendeleo kwa sababu uchumi wake uko imara na inakopesheka

Dkt. Tadesse ametoa ahadi hiyo Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango ambapo wawili hao wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo hususan Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na ujenzi wa mradi wa kufua umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya mto Ruhudji mkoani Njombe

Amesema kuwa miezi michache iliyopita Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola bilioni 1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele inayotekelezwa na Serikali na kwamba wako mbioni kutoa kiasi kingine kikubwa cha fedha hivi karibuni.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Benki hiyo ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika TDB imekuwa mdau muhimu katika maendeleo ya Taifa na kwamba pamoja na kiasi cha dola bilioni moja kilichopokelewa na Serikali mwezi Agosti Mwa huu 2019, Serikali inatarajia kupata kiasi kingine cha dola milioni 300.

Amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kati ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) pamoja na miradi ya kuzalisha nishati ya umeme ili nchi iweze kuimarisha sekta ya uzalishaji viwandani kwa kuwa na umeme wa uhakika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua akizunguza wakati wa kikao na Rais huyo wa TDB amesema kuwa amefurahi kwamba Benki hiyo imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Ruhudji (MW 358) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 460.2 ambapo kati ya hizo dola milioni 407 zitatumika kujenga mitambo ya kufua umeme na kiasi kingine cha dola milioni 53 kitatumika kujenga njia ya kusafirishia umeme urefu wa km 170.

Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2025 na kwamba kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kufikia azma hiyo ili kuimarisha masuala ya uzalishaji viwandani na uendeshaji wa miundombinu mingine inayotumia nishati hiyo ya umeme.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amemweleza Rais huyo wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Admassu Tadesse kwamba ujenzi wa kipande cha Reli ya Kisasa kati ya Dar es Salaam na Morogoro umefikia asilimia 72 hivi sasa na kuishukuru Benki hiyo kwa utayari wake wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli kipande cha Mwanza hadi Isaka.

Tanzania ni mongoni mwa wanahisa 31 wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini Mwa Afrika (TDB) ambapo hadi kufikia Disemba 31 mwaka 2018, Tanzania ilikuwa imeshika nafasi ya 4 ya uwekezaji katika Benki hiyo ikiwa na asilimia 8.33 ya hisa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: