Mtaalam wa Mawasiliano kutoka UNICEF Tanzania, Usiah Nkoma akitoa mada katika semina ya wahariri iliyofanyika katika Hoteli ya Regency kwa ajili ya kusaidia kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama yenye lengo la kuzuia vifo vya mama wajawazito na watoto.
Kaimu Mratibu Wa Afya ya Mtoto katika mkoa wa Dar as Salaam, Agnes Mgaya akitoa mada katika semina ya wahariri juu ya kusaidia kuokoa Vigo vya mama na mtoto.
Mmoja wa wahariri, Peter Nyanje akichangia katika semina ya wahariri iliyokuwa inahusu kusaidia kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama yenye lengo la kuzuia vifo vya mama wajawazito na watoto.
Baadhi ya wahariri kutoka vyombo mbalimbali wakiwa katika semina iliyokuwa inahusu kusaidia kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama yenye lengo la kuzuia vifo vya mama wajawazito na watoto.
Mtaalam wa Mawasiliano wa UNICEF Tanzania Usiah Nkoma, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa semina iliyokuwa inahusu kusaidia kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama yenye lengo LA kuzuia vifo vya mama wajawazito na watoto.
Shirika la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) Tanzania limesema vifo vya watoto wachanga na mama wajawazito ni miongoni mwa changamoto inayozikumba nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.
Kufuatia hali hii, shirika hilo limesema wadau, wakiwemo wahariri ,waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wana nafasi ya kuelemisha jamii, ili kusaidia mama wajawazito na watoto wachanga kuepuka vifo zisivyo vya lazima wakati na baada ya kujifungua.
Mtaalamu wa Mawasiliano wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Tanzania, Usiah Mkoma amesema katika semina ya wahariri, iliyoandaliwa na kampuni ya True Vision Production kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na UNICEF katika hoteli ya Regency iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam kuwa wahariri kutoka vyombo vya habari nchini wanaweza kutumia nafasi zao na kalamu zao katika kusaidia kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kumsaidia mama mjamzito kwenda kliniki ili avuke salama yeye na mtoto atakayemzaa.
Umbali, hali duni ya miasha, ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, mila na desturi potofu ni miongoni mwa sababu zinazopelekea vifo hivyo, kwa mujibu wa Agnes Mgaya, ambaye anakaimu nafasi ya uratibu wa Afya ya Mtoto mkoa wa Dar es Salaam. Mkoma amesema akina mama wajawazito 8,200 hufa kila mwaka wakati wakijifungua na asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka 5 hufa pia kila mwaka ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa kwa changamoto mbalimbali.
Hivyo amesema wahariri wana wajibu wa kuelimisha jamii, kutumia kalamu zao kuelezea umuhimu wa kwenda kliniki wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.
“Muhimu ni kuhakikisha ndani ya siku 42 baada ya kujifungua, mama aendelee kuwa chini ya uangalizi wa wataalam wa afya ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoweka kujitokeza kama vile kifafa cha mimba,’ amesema Nkoma.
“Tutumie vyombo vyetu vya habari kuchochea habari zinazowahusu mama mjamzito na mtoto mchanga ili kupunguza vifo vyao visivyo vya lazima,”
“Kwa kufanya hivyo, tutawafanya watunga sera na watendaji wachukue hatua za haraka”, amesema Mkoma.
“Mbali na vyombo vya habari mnavyoviongoza, pia nawaomba mtumie akaunti zenu binafsi za mitandao ya jamii kuwa sehemu ya kampeni ya kuzuia vifo zinavyotokea hapa nchini,” ameongeza.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza katika vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na changamoto mbalimbali za uzazi, zikiwemo kutokwa na damu nyingi wakati na baada ya kukifungua, ukosefu wa chanjo na umbali wa vituo vya afya katika baadhi ya maeneo.
Nchi nyingine ni India, Bangladesh, Nigeria, Jamhuri ya Watu wa Congo, Ethiopia, China na Palestina.
Amesema kutokana na takwimu kuonyesha vifo vipo juu, UNICEF Tanzania inashirikiana na wadau , ikiwemo serikali, taasisi na mashirika katika kuhakikisha mama na mtoto wanavuka salama katika kipindi cha uzazi.
Akizungumza katika semina hiyo, mmoja wa wahariri na waandishi wakongwe, Theophil Makunga amesema takwimu za vifo vya mama wajawazito na watoto zinatisha, hivyo ni muhimu waandishi wakatumia kalamu zao kuhakikisha vifo hivyo havitokei.
“Kazi ya waandishi wa habari ni kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, hivyo katika maeneo haya matatu, kuelimisha jamii ni kazi yetu,”
“Hivyo nadhani wajibu wa waandishi sio tu kuandika habari mbaya, bali pia wajibu kuandika habari zinazohusu maendeleo ya jamii na kutoa suluhisho la matatizo yanayojitokeza ili hatua zichukuliwe na jamii, watendaji na watunga sera,” amesema Makunga.
Pili Mtambalike, miongoni mwa waandishi wakongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali katika Baraza la Habari Tanzania (MCT) amesema ana imani mtazamo wa vyombo vya habari katika kuandika habari zinazowahusu mama wajawazito na watoto utabadilika, baada ya semina hii.
“Siku zote, habari zinazohusu siasa, watu maarufu zimekuwa zikichukua nafasi sana katika vyombo vyetu vya habari, lakini, nina Imani, semina hii itasidia kubadilisha fikra za wahariri wengi na kutoa kipaumbele pia katika habari zinazowahusu mama wajawazito na watoto katika maeneo yao ya kazi,” amesema Mtambalike.
TVP, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na UNICEF, imeandaa semina tatu kwa kada tofauti katika kuhakikisha jamii inaelimishwa juu ya umuhimu wa kuwasaidia mama wajawazito na watoto wavuke salama.
Takwimu zinaonesha asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka 5 nchini Tanzania hufariki ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa. Wanawawake wajawazito 8,200 hufariki kwa mwaka wakati wakijifungua.
Moja ya malengo ya Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ni kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, kutoka 556 mpaka 292, kama sio kumaliza kabisa ifikapo mwaka 2020.
Pia kampeni imeweka malengo ya kuokoa vifo vya watoto wachanga kutoka 43, mpaka 25 kwa vizazi hai 1,000 ifikapo mwakani.
Baada ya semina ya wahariri, kesho (23/04/2019) kutakuwa na semina itakayohusisha viongozi wa dini katika ukumbi wa hoteli ya Regency, iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Semina ya mwisho itafanyika Ijumaa, ikiwahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya Taifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.
Madhumuni ya Serikali ni kuhamasisha viongozi wake, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya serikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujumla kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: