Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) iliyofanyika Jengo la Takwimu tarehe 13 Aprili, 2019 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizindua Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey). (Kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko, Naibu Waziri wa Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman. (Kulia) ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya, Mhe. Osca Mukaza
Naibu Waziri wa Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman akieleza namna Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa zikishirikiana katika kukabiliana na Ugonjwa wa Ukimwi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko akitoa maelezo mafupi kuhusu utafiti huo uliofanyika juu ya Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) iliyofanyika Jengo la Takwimu tarehe 13 Aprili, 2019 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa pamoja na viongozi wengine wakifuatilia ripoti fupi iliyokuwa ikiwasilishwa na mwakilishi kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) hayupo pichani. (Wa pili kutoka kushoto) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stalla Ikupa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akionesha kitabu cha Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) baada ya kuzindua taarifa hiyo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi kitabu cha Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) Bi. Dorothy Mwaluko mara baada ya Kuzindua taarifa hiyo, Aprili 13, 2019 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi na wadau wa maendeleo mara baada ya kuzindua Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) Jijini Dodoma. PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU).
Na; Mwandishi Wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amezindua taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi wa mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) tarehe 13 Aprili, 2019 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo alieleza kuwa utafiti huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali imeendelea kupambana na ugonjwa wa Ukimwi kwa kuonesha juhudi za kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya na kupungua kwa vifo vinavyotokana na Ukimwi.
“Tafiti zinaonesha maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000 kwa mwaka katika mwaka 2017, vilevile takimu zinaonesha kupungua kwa vifo vinavyotokana na Ukimwi kutoka watu elfu 70 kwa mwaka katika 2010 hadi kufikia vifo elfu 32 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2017,” alieleza Mhagama
Alisema kuwa katika kuthibitisha hilo, kiwango cha maambukizi ya Ukimwi nchini kinazidi kupungua ambapo mwaka 2012 matokeo ya utafiti kama huo yalionesha kuwa kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 na matokeo ya mwaka 2016 – 2017 kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7.
Waziri Mhagama alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa watu waliopima afya zao kwa hiari wanaongezeka kutoka tafiti moja hadi nyingine, kati ya watu hao wanawake waliopima ni wengi kuliko wanaume.
Sambamba na hilo, amewapongeza wanawake kwa ujasiri na moyo wa kujali afya zao, pia kuwahimiza wanaume kujitokeza kwa wingi kupima ili wafahamu hali zao za kiafya.
Hata hivyo, Waziri Mhagama ametaka kila Mkoa na Halmashauri zote nchini kujadili matokeo ya utafiti huo kwa undani katika kamati za VVU na Ukimwi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji ili kuelewa hali ilivyo katika maeneo yao na kuandaa mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la maambukizi mapya ikiwemo kuongeza upatikanaji wa huduma stahiki kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Aidha, alitoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi na kupima afya zao, pia jamii kuelimishwa na kuhamasishwa juu ya umuhimu wa kutumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Aliongeza kwa kuagiza TACAIDS na Baraza la Watu wanaoishi na Ukimwi (NACOPHA) kuongeza jitihada dhidi ya unyanyapaa na ubaguzi.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman alisema kuwa taarifa ya utafiti huo itasaidia watunga sera na waratibu wa miradi kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi iliyopo kuandaa mikakati mipya kuhusiana na masuala ya Ukimwi hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko alisema kuwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania imekuwa ikiratibu zoezi hilo la utafiti kila baada ya miaka mine na tafiti tatu zimeshafanyika mwaka 2003 – 2004, 2007 – 2008 na 2011 – 2012.
Pia, Kaimu Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa malengo ya msingi ya utafiti utafiti huo yalikuwa ni kutoa makadirio ya mwaka ya Kitaifa ya maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64, na kutoa makadirio ya hali halisi ya upimaji wa VVU Kitaifa na Kimkoa.
“Utafiti wa aina hii ni wa kwanza kufanyika hapa nchini kwa kuwa umeangalia vitu vingi na umeshirikisha watu wa rika lote na viashiria vingine tofauti na tafiti nyingine zilizofanyika hapo awali,” alisema Chuwa.
Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi na Matokeo yake wa Mwaka 2016 – 2017, ulitekelezwa kwa kushirikiana baina ya Ofisi ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar na ICAP Tanzania, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Afya – Zanzibar na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (ZAC), Maabara ya Taifa ya Afya za Jamii, Uhakiki, Ubora na Mafunzo, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), na Kitengo Shirikishicha Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma, Zanzibar (ZIHTLP) kwa kushirikiana na wadau kutoka shirika lisilo la Kiserikali Centers for Disease Control and Prevention (CDC).
Toa Maoni Yako:
0 comments: