Mkurugenzi wa Kitengo cha Mazingira Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Mhandisi Modester Mushi akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji na kurudisha ubora wa maeneo pindi miradi inapomalizika leo kwenye Kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
MKURUGENZI wa Kitengo cha Mazingira Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) Mhandisi Modester Mushi amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kulinda vyanzo vya maji.
Hayo ameyasema wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji yaliyofikia tamati leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Mhandisi Modester amesema mazingira yanatakiwa yalindwe katika nyanja zote kuanzia kwenye vyanzo vya maji, miradi inayojengwa na kupata ushauri kutoka Baraza la Mazingira NEMC na Wizara husika.
Amesema, katika sheria ya mazingira ya 2004 imeweka wazi kuwa kwenye kila mradi uandaliwe tathimini itakayoangalia athari za kijamii na kibinadamu. “Mkandarasi anatakiwa afahamu mazingira anayoenda kufanyia kazi, wafanyakazi kuwa na vifaa vya kufanyia kazi, alama elekezi zitakazomuonyesha mwananchi kazi inayofanyika kwa muda huo,”amesema Modester.
Ameeleza, miradi inapomalizik basi hali ya mazingira inatakiwa irudishwe kama awali au kuboreshwa zaidi ya zamani na hilo linakuja mpaka upande wa uendeshaji wa mfumo wa majitak ikiwemo kuandaa sheria. Akizungumzia upandaji wa miti pembezoni mwa vyanzo vya maji, Mhandisi Modester amesema wameshapanda miti 23,000 aina ya mitomondo katika Chanzo cha Mto Kizinga, pembezoni mwa mto Ruvu kuanzia kwenye Mtambo wa Ruvu Chini na zoezi hilo litaenda mpaka Mgeta chanzo kilipoanzia.
Amesema, upandaji wa miti unapunguza mmomonyoko wa ardhi na kusaidia ardhi kushika na shughuli za kijamii zinazofanyika pembezoni za Mto husababisha udongo kuingia na kiwango cha tope kuwa kingi na kupelekea kina cha mto kupungua na kusababisha mafuriko.
Ameongezea na kuwataka wananchi watunze mazingira ili yawatunze na kuwaomba washirikiane na Maafisa ugani ambao ni wataalamu wa kilimo ili kuweza kutambua ni aina gani ya udongo na mimea inayofaa kupandwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: