Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akionyesha tuzo yake baada ya kupokea tuzo hiyo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri kwa mwaka 2019 katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo na Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump juzi jijini Washington, D.C. Anna Henga anakuwa ni Mtanzania wa pili kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri, akifuata nyayo za Vicky Ntetema aliyepata tuzo hii mwaka 2016. (Picha: Ubalozi wa Marekani).

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Anna Henga ametunukiwa Tuzo ya Mwanamke jasiri duniani kwa 2019 kutokana na utetezi wa haki za binadamu. Tuzo hizo zilizotolewa na Ikulu ya Marekani zilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo na kuhudhuriwa na Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump.

Katika hafla hiyo Pompea alihimiza umuhimu wa kutambua mchango wa wanawake wanaoonesha juhudi zao popote duniani katika kupambana na changamoto zinazozaa matunda. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani kupitia tovuti yake tuzo hizo hutolewa kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake 10 jasiri na wenye uthubutu katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Henga ni moja ya wanawake ambaye juhudi zake katika utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania ni za mfano. Wanawake wengine tisa waliotunukiwa tuzo hiyo wanatoka katika mataifa ya Bangladesh, Burma, Djibouti, Egypt, Jordan, Ireland, Montenegro, Peru na Sri Lanka.

Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2007 ni kutambua mchango wa wanawake wanaojitoa kwa nguvu na ujasiri kama viongozi katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii. Mpaka sasa kupitia tuzo za IWOC, Ikulu ya Marekani imetambua mchango kwa wanawake zaidi ya 120 kutoka nchi zaidi ya 65 katika kutetea haki za binadamu, kudumisha nafasi ya wanawake katika jamii na kudumisha amani na utawala bora katika nchi zao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: