Lengo la ziara hiyo ni kupata taarifa ya maandalizi, kukagua timu hizo na kuwatia hamasa katika kuelekea katika Mashindano ya Majeshi yatakayoanza kutimua vumbi kesho Jumamosi Februari 23. Michezo hiyo ya Majeshi hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).
Akitoa taarifa ya Maandalizi na hali za wachezaji, Mwenyekiti wa BAMMATA Kanda ya Uhamiaji Naibu Kamishna wa Uhamiaji Nasra Jumaa alimweleza Kamishna Jenerali kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na wana ari ya kushindana.
“Afande Kamishna Jenerali tunashukuru kwa ujio wako hapa na napenda kukujulisha kuwa wachezaji wako katika hali nzuri, wana ari kubwa na wako tayari kuiletea ushindi na heshima idara yetu ya uhamiaji. Tunakuahidi ushindi tu” Alisema Naibu Kamishna Nasra.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala leo tarehe 22 Februari, 2019 amefanya ziara ya kuwatembela Wachezaji wa Timu za Mpira wa Miguu na Kikapu walioweka kambi katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es salaam.
Naye Mwalimu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Uhamiaji maarufu kama Kimbunga FC, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Wahid Mmanga akitoa taarifa kuhusu timu yake alisema kwamba wako tayari kupambana na kuleta ushindi dhidi ya timu nyingine za Majeshi kwani safari hii hawatokubali kuwa wasindikizaji.
“Afande sie tumekuja kucheza ili tushinde, miaka iliyopita timu kutoka majeshi mengine walikuwa wakitumia wachezaji wa Timu zao ambazo ziko Ligi Kuu lakini kwa utaratibu mpya mwaka huu hakuna kutumia wachezaji wa timu za majeshi zilizo Ligi Kuu ya soka Tanzania hivyo tuna uhakika wa kuchukua kikombe” Alieleza Naibu Kamishna Mmanga.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Makakala alieleza kuridhishwa na maandalizi ya timu na kuwatakia wachezaji kila la kheri kwenye Mashindano hayo. “Nimefurahishwa na maandalizi, mnaonekana kweli mna ari na hamasa ya ushindi. Naomba mkacheze ili kuiletea heshima idara yetu, mimi na watumishi wote wa Uhamiaji tuko pamoja nanyi na tutawashangilia kila mnapocheza. Hii michezo inasaidia sisi kama jeshi la uhamiaji kujenga mahusiano mazuri na majeshi mengine ya nchi yetu, pia ni faida kwenu wachezaji kwani inawajengea afya bora kwa mazoezi mnayofanya. Niwatakie kila la kheri”.
Michezo ya Majeshi kwa mwaka huu itashirikisha timu za wachezaji wa Mpira wa Miguu, Kikapu, Kuvuta Kamba, Kulenga shabaha na Riadha. Michezo hiyo itafunguliwa rasmi kesho Jumamosi saa nne asubuhi katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments: