Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdediti Kakoko, akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Fredy Lihundi, akifafanua jambo
Wakandarasi wanaofanya upanuzi katika Bandari ya Dar es Salaam, wakijadili jambo katika mradi huo na viongozi wa TPA.
Mtambo wa kuchimba kina cha Bahari ukimwaga mchanga nje ya bahari katika Bandari ya Dar es Salaam.
Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
Upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umefikia hatua nzuri baada ya kukamilka kwa upanuzi wa gati namba moja kwa asilimia 100 huku meli ya kwanza ikitarajiwa kutia nanga wiki moja ijayo ikishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdediti Kakoko, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa Sh. bilioni 336.7 wa upanuzi wa bandari hiyo.
Amesema upanuzi huo umeiongezea uwezo gati hiyo yenye urefu wa mita 192 wa kubeba meli kubwa mbili za tani 45,000 hadi tani 60,000 kwa wakati mmoja kutokana na kuongezewa kitako cha upana wa mita 11.5 kinachobebwa na nguzo imara za zege zilizochimbiwa mita 70 chini ya bahari.
Amesema baada ya mkandarasi kukabidhi gati hiyo siku chache zijazo atakabidhiwa na kuanza kazi ya upanuzi wa gati namba mbili inayotarajiwa kukamilika Machi mwakani na upanuzi utaendelea hadi kufikia gati namba saba.
Akizungumzia ujenzi wa gati ya magari (RoRo Berth) pamoja na yadi ya kuegesha magari amesema mradi huo ulitakiwa uwe umekamilika lakini mkandarasi alikutana na changamoto ya kuwepo kwa udogo mbaya na hivyo kulazimika kutafuta udogo mzuri na kuujaza na kwamba ujenzi unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Juni mwakani.
Kakoko amesema kukamilika kwa gati hiyo kutaiwezesha bandari hiyo kupokea magari 10,000 kwa siku kutoka uwezo wa kupokea magari 2500 na kwa mwaka itakuwa magari 200,000 kutoka magari 90,000.
"Kukamilika kwa gati hii kutaleta mapinduzi makubwa kwani tunàweza kupokea meli ya magari 3000 hadi 5000 na ikapakuliwa kwa siku moja tu," amesema na kusisitiza;
"Ndugu wananchi na wadau hasa mawakala wa meli wakae mkao wa kula waachane na siasa za kuambiwa meli zina subiri sana hapa tuna meli 12 tu na zilishawahi kufika 18 tu naomba wananchi wawe na amani serikali yao inafanya kazi."
Ameongeza kuwa upanuzu wa gati utaenda sambamba na upanuzi wa lango la bandari kwa kuongeza kina kutoka mita 10 hadi 16 ambapo kwa sasa unafanyika usanifu na ifikapo Juni mwakani uchimbaji utaanza rasmi.
"Nia yetu ni hadi kufikia Disemba mwakani tuwe na gati kuanzia sifuri hadi namba tatu na upanuzi wa lango uwe umekamilika ili tuweze kupokea meli za kimataifa zenye kina cha mita 15 na uwezo wa kubeba hadi makasha 6000 kutoka meli za sasa zinazoweza kubeba makasha 2500 tu," alisema Kakoko.
Aliongeza, "Watu wa meli wajiandae hapa meli zitakuwa zinapishana kama daladala zinavyopishana, bandari hii ipo kwenye eneo ambalo Mungu amelibariki kijografia katika ukanda huu kuanzia Misri hadi Afrika Kusini na kwa sasa biashara ya dunia imehamia upande wa Mashariki kutoka Magharibi.
"Hivyo miaka mitatu ijayo tuna uhakika wa kurudisha ule utukufu wa bandari ya Dar es Salaam," alisisitiza.
Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi TPA, Charles Ogale, alisema mradi huo unahusisha uongezaji wa kina cha kutoka mita sita hadi mita 12.9 kutoka usawa wa bahari baada ya maji kupwa, upana wa mita 34 na itakuwa na urefu wa mita 320 pamoja na ujenzi wa yadi yenye ukubwa wa mita za mraba 69,000.
Alisema mradi mzima wa upanuzi wa gati ya magari ambayo ni 'zero berth' hadi gati namba saba ulioanza Juni 2017 unatarajiwa kukamilika Juni 29 2020.
"Upanuzi huu umeiongezea gati uwezo wa kubeba meli kubwa zaidi pasipo kupata misukosuko yeyote ," amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: