Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Radhiya Rashid Haroub (kushoto), wakati wa Kikao cha kubadilishana uzoefu juu ya suala la ufungaji wa kamera maalumu za kuzuia na kudhibiti uhalifu ambazo tayari zimeshafungwa Visiwani Zanzibar. Wengine ni ujumbe kutoka Jeshi la Polisi ulioongozana na Naibu Waziri, ukiongozwa na Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi, SACP Saleh Mohamed Saleh (watatu kushoto).Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Radhiya Rashid Haroub akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, wakati wa Kikao cha kubadilishana uzoefu juu ya suala la ufungaji wa kamera maalumu za kuzuia na kudhibiti uhalifu ambazo tayari zimeshafungwa Visiwani Zanzibar. Wengine ni ujumbe kutoka Jeshi la Polisi ulioongozana na Naibu Waziri, ukiongozwa na Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi, SACP Saleh Mohamed Saleh (watatu kushoto).Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekutana kujadili suala la ufungaji kamera maalumu za kudhibiti na kuzuia uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alisema Serikali inatambua umuhimu wa ulinzi na usalama kwa raia wake na iko katika mpango wa kufunga kamera hizo katika miji yote mikuu nchini.
Waziri Masauni alisema lengo la kufunga kamera hizo ni kuiwezesha serikali kupambana na matukio ya uhalifu ya utekaji, makosa ya barabarani, uporaji wa fedha katika taasisi za fedha.
“Tumekuja kuchukua uzoefu kwa wenzetu wa Zanzibar ambao tayari wameshafunga kamera hizi katika maeneo mbalimbali na nimeona jinsi zinavyofanya kazi za kubaini wahalifu.
“Teknokolojia haiepukiki katika kudhibiti, Serikali tumejipanga na hivi karibuni tutaanza kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu na maeneo ya mikoa iliyoko mipakani ili kudhibiti wahalifu kutoka nje ya Tanzania,” alisema Masauni
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Radhiya Rashid Haroub alisema tayari washafunga kamera hizo ambazo zilizinduliwa Oktoba 3, mwaka huu.
Alisema uzinduzi wa kamera hizo ulifanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
“Mfumo huo ni muhimu na tumehakikisha unaimarisha usalama katika mji wa Zanzibar ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa amani na salama na tayari ushaanza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali hapa Zanzibar,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: