Wafanyakazi watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakiwa wamefishwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi
Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
WAFANYAKAZI watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais -Muungano na Mazingira Januari Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.
Wakili wa Serikali Faraja Nguka amewasomea washtakiwa makosa yao leo Oktoba 31, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando.Wakili Nguka amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 160 milioni.
Aidha Mahakama imetoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa Magori Wambura (38) mkazi wa Bombambili kwa sababu wakati washtakiwa hao wakisomewa mashtaka hayo yanayowakabili mshtakiwa huyo ambae ni Ofisa mazingira wa Nemc, hakuwepo mahakani.Wakili Nguka amewataja washtakiwa hao kuwa ni Ofisa wa Mazingira NEMC Deusdith Katwale, Msewe, Luciana Lawi, Edna Lutanjuka, Ofisia Mwaruka na Lilian Laizer.Imedaiwa kati ya Septemba 27, 2016 na April I mwaka huu wa 2018 washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.
Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa, Oktoba 17,2017 kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati wakijua si kweli.Pia washtakiwa hao wanadaiwa kughushi saini ya Januari Makamba ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais -Muungano na Mazingira katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati wakati wakijua si kweli.
Mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba 2017 katika ofisi za NEMC Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 cha oktoba 17,2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati akijua si kweli.
Pia washtakiwa walijipatia kwa njia ya udangnyifu Sh.milioni 160 toka kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangefanya tathimini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na NEMC kitendo ambacho si kweli.Aidha washtakiwa wanadaiwa kati ya Septemba 27, 2016 na Aprili 6,2018 Dar es Salaam waliisababishia NEMC hasara ya Sh.milioni 160.
Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu,.Washtakiwa wamepelekwa rumande kesi imeahirishwa hadi Novemba 14, mwaka huu na upelelezi wake bado haujakamilika.
Toa Maoni Yako:
0 comments: