Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira wa Nipe Fagio, Bi Ana Rocha (kulia) akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam juu ya mradi wa kimataifa wa uhifadhi wa Mazingira ya Asili wa “Interact Bio”. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira wa Nipe Fagio, Bi Ana Rocha (kulia) akiwaonyesha waandishi wa habari Bustani wima ambayo imetengenezwa kutokana na fremu za mbao,chuma, mbolea na chupa za plastiki, na Kifaa cha Makazi ya wadudu ikiwa ni Mradi wa kimataifa wa uhifadhi wa Mazingira ya Asili wa “ Interact Bio”.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira wa Nipe Fagio, Bi Ana Rocha (Kulia) wakionyesha bango linaloonyesha umuhimu wa uoto asili katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha na Moshi, (Kushoto) ni Afisa Tehama wa Taasisi ya Nipe Fagio Olarip Tomito.
Moja ya bustani za wima iliyotengenezwa na inazotarajiwa kufundishwa kwa wananchi ili zichangie katika utunzaji wa mazingira.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mradi wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira Asili wa (Interact-Bio) chini ya Baraza la Kimataifa la Mazingira utashiriki katika maonyesho ya sekta ya ujenzi yatakayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam kuanzia kesho kwa lengo la kuonyesha njia za kiubunifu za kuwawezesha wakazi wa mijini kunufaika na viumbe na mazingira asilia.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira ya Nipe Fagio, Bi. Ana Rocha amesema leo kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba mradi huo umejenga bustani ya wima, gudulia la kuhifadhia mbolea na kifaa cha makazi ya wadudu (insect hotel) ili kuwawezesha wakazi wa jiji la Dar es Salaam watakotembelea maonyesho hayo kujionea namna ya kujumuisha na kunufaika na viumbe asili katika maisha ya mijini.
“Tunashirikiana na Halmashauri za Miji katika jitihada za kuongeza uelewa kuhusu manufaa yatokanayo na viumbe asili katika majiji ya Dar es salaam na Arusha pamoja na manispaa ya Moshi. Tunataka wananchi waone thamani ya kuwa na viumbe asili katika jiji na jinsi ambavyo jambo hili linaweza kutatua changamoto ya ongezeko la joto na changamoto nyingine zinazowakabili wakazi wa mijini kutokana na mabadiliko ya mazingira pamoja na hali ya hewa”.
Amesema bustani wima ni bustani ambayo inatengenezwa kutokana na fremu za mbao, chuma, mbolea na chupa za plastiki kuotesha maua na mboga mboga kwenye kuta za nyumba au nguzo ikiwa ni njia mbadala wa kupanda mimea hiyo ardhini. Mbinu hii ya ubunifu inaweza kutumika kuweka mpaka wa mimea kati ya maeneo tofauti na kutoa nafasi kwa mimea hiyo kustawi huku ikiwasaidia wakazi wa mijini kutumia vizuri nafasi ndogo waliyonayo kwa ajili ya bustani.
Rocha amesema bustani hizo zina manufaa mengi ikiwemo kusaidia kupunguza joto kwenye majengo kutokana na uwezo wa mimea kubadilisha hali ya hewa huku ikisaidia upatikanaji wa makazi kwa ndege na viumbe hai wengine. Vilevile amesema bustani hizi zinaweza kuwa chanzo endelevu cha chakula kwa binadamu kwa zinaweza pia kutumika kuzalisha mboga na matunda.
Akizungumzia kuhusu kifaa maalum ambazo ni makazi ya wadudu wenye faida, Rocha alisema kwamba kifaa hicho kimetengenezwa mahususi kuweza kuwavutia wadudu wenye faida kwa viumbehai. Tumejenga kihota cha kuwavutia wadudu na kinajulikana kama “insect hotel” kwa ajili ya vipepeo na tutakitumia kuonyesha ni jinsi gani wadudu wana umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku hasa katika kuvunja vunja na kuteketeza taka na vile tutaonyesha ni jinsi gani wadudu hawa wanaweza kuwa chakula kwa ndege na wanyama wengine.”
Vilevile Rocha alifafanua kwamba katika maonyesho hayo, magudulia maalum ya mbolea ambayo yanaweza kutengenezwa kwa mbao, ndoo zilizotumika na chuma yataonyeshwa na kuongeza kuwa magudulia hayo yametengenezwa mahususi kwa ajili ya kuwawezesha wakazi wa mijini kutumia taka zitokanazo na chakula kama mbolea kwa ajili ya kurutubisha udongo wa bustani jambo ambalo pia linapunguza gharama za kupeleka taka dampo.
Kwenye maonyesho hayo, wageni wataweza kujionea na kujifunza mbinu nyingine mbalimbali za kujumuhisha mazingira na viumbe asili katika maisha ya mijini.
Toa Maoni Yako:
0 comments: