Benki pamoja na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na utoaji wa mikopo hapa nchini zimetakiwa kuwa na kitengo maalum cha kumshauri mteja wake kabla ya kukopa, ili kupunguza wimbi la wateja wanaofilisiwa baada ya kushindwa kurejesha pesa wanazodaiwa na benki husika.
Wananchi kutoka kata mbalimbali za jiji la Dar es salaam wakifuatilia semina.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wananchi walioshiriki katika semina ya GDSS mapema jijini Dar es salaam, ambapo wananchi wengi wamezitupia lawama benki nyingi kwa kudai kuwa maafisa wake hawana utu wala huruma katika kudai madeni yao.
Lakini pia imeelezwa kuwa lugha inayotumiwa na benki zote sio rafiki kwa wateja wengi kwani inasababisha wananchi kujiingiza katika majanga makubwa bila wenyewe kujijua, na kuombwa ikiwezekana itumike lugha ya Kiswahili kwani sio wananchi wote wanaelewa kingereza.
Mwananchi kutokea kata ya Kipunguni Selemani Bishagazi akichangia mada na kuonyesha msisitizo juu ya kile anachokiamini yeye.
Akiongea katika semina hiyo Mwanaharakati kutoka Kipunguni Bw. Selemani Bishagazi alisema kuwa kinachowaponza wananchi wengi ni kukopa kwa shida sio kukopa kwa malengo ya kukuza au kuendeleza biashara ndio sababu inayowafanya kuyumba na hatimaye kufilisiwa na benki au taasisi za mikopo.
Aliongezea kuwa benki nyingi zinafurahia kuona mteja anashindwa kulipa deni ili wachukue mali yake aliyoweka rehani, kwani kwa sasa taasisi nyingi za mikopo zinaangalia kupata faida kubwa kupitia kwa wananchi wanyonge na wasiojua nini kimeandikwa katika mkataba wanaouingia kati yao na benki na sio kuwasaidia.
Mwanaharakati Janeth Mawinza akitoa maoni yake kuhusiana hali halisi ya mikopo ya biashara mingi hapa nchini.
Kwa upande wake Dada Janeth Mawinza kutoka Mwananyamara alisema kuwa kinachowaumiza wanawake wengi ni kukosa elimu ya biashara kwani unakuta mwanamke anakopa pesa baada ya kufanyia biashara anakwenda kulipia sherehe au ada ya mtoto shule bila kuwa na mipango ya kuangalia atarejeshaje pesa hiyo na wakati haizunguki.
Lakini pia kingine ni kwamba biashara moja ina mkopo zaidi ya mmoja mkopo wa kwanza unachukuliwa ukishindwa kuendesha biashara anaenda kwenye benki nyingine anachukua pesa kwenda kulipa deni na huo ukishindwa tena anakopa tena kuja kulipa madeni ya nyuma hali inayofanya mkopaji kushindwa kwenda mbele na matokeo yake kufilisiwa mali zake.
Na mwisho maafikiano ni kuwa elimu itolewe kwa Maafisa Mikopo juu ya kuwaelimisha wateja wao na namna ya kudai wateja wao, na elimu hii itolewe na Benki kuu ya Tanzania (BOT) ambao ndio wasimamizi wakubwa wa taasisi za kifedha.
Toa Maoni Yako:
0 comments: