Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Mwantyala akiongoza mamia ya watu (hawapo pichani) waliokusanyika katika ibada maalum ya kumuomba Mungu aiepushe Tanzania na majanga mbalimbali zikiwemo ajali za mara kwa mara. Kupitia ibada hiyo iliyofanyika jana makao makuu ya huduma hiyo yaliyopo Yespa mjini Kihonda Mkoa wa Morogoro, pia alitoa salamu maalum za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na Watanzania wote kutokana na ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu huko Ukerewe mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya abiria zaidi ya 200 huku kadhaa wakijeruhiwa.
Baadhi ya umati wa Watanzania waliokusanyika katika ibada maalum ya kumuomba Mungu aiepushe Tanzania na majanga mbalimbali zikiwemo ajali za mara kwa mara katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania inayoongozwa na Nabii Joshua Mwantyala (hayupo pichani) wakiendelea na maombi jana, Yespa mjini Kihonda Mkoa wa Morogoro. Nabii Joshua kupitia ibada hiyo alitoa salamu maalum za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Watanzania wote kutokana na ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu huko Ukerewe mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya abiria zaidi ya 200 huku kadhaa wakijeruhiwa.
*Mungu aliepushe na ajali, atoa salamu za pole kwa Rais Dkt. Magufuli, Watanzania

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania,Nabii Joshua Mwantyala ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Jonh Magufuli kutokana na maafa yaliyosababishwa na kuzama kwa Kivuko cha MV. Nyerere Septemba 20,mwaka huu.

Katika ibada maalum iliyowakutanisha maelfu ya Watanzania makao makuu ya huduma hiyo yaliyopo Yespa mjini Kihonda mkoani Morogoro jana, mbali na kutoa salamu hizo pia walifanya maombi maalum ili Mungu aepushe mbali ajali mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea nchini.

"Tunapenda kutoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba uliotokana na ajali ya kuzama Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Ziwa Victoria, Ukara wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza Septemba 20, mwaka huu.

"Msiba huu umegusa kila mmoja, kwetu sisi Sauti ya Uponyaji, tumeona tuzidi kumuomba Mungu ili aendelee kulilinda Taifa letu, maana maadui, shetani wanatujaribu kila siku ili kutuyumbisha, jambo ambalo halitawezekana maana, sisi tuliotakaswa kwa damu ya Yesu tumepewa mamlaka ya kuharibu, kung'oa na kuteketeza ngome zote za muovu shetani, hivyo, tuzidi kumshirikisha Mungu kila jambo maana yote yanawezekana,"alifafanua Nabii Joshua.

Pia Nabii Joshua alimuomba Rais Dkt. Magufuli kutokata tamaa au kuyumbishwa na viongozi wazembe ambao kwa namna moja au nyingine utendaji kazi wao umekuwa wa kimazoea, badala yake aongeze nguvu maana aliyempa nafasi hiyo ni Mungu ili aweze kuwatumikia Watanzania kwa moyo, hekima na maarifa bila kuchoka.

Alisema, ili kuhakikisha ulinzi wa Mungu unatawala kila kona ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania inaendelea na Kampeni ya Ombea Taifa ikiwemo mpya ilioanza hivi karibuni ya siku 90 ya Operesheni Rudi kwa Baba.

Nabii Joshua alisema, kupitia kampeni hizo, maelfu ya watu watashirikiana kuliombea Taifa ili Mungu aweze kuachilia baraka zake kuanzia uchumi, afya, ulinzi, maendeleo, usalama barabarani, angani, majini ikiwemo elimu, uchumi wa viwanda na nyingine nyingi.

Katika hatua nyingine alisema, katika ibada hizo kila atakayeshiriki atarajie kuuona ukuu wa Mungu, kwani atapokea uponyaji wa papo kwa papo na mahitaji yake pia Mungu atayapa majawabu.

Pia alitoa wito kwa watumishi wote wa umma na binafsi kufanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo ya Taifa, kwani hakuna mafanikio bila bidii katika kazi ikiwemo kumtanguliza Mungu mbele.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: