Na Derek Murusuri.

AKIWA anafundisha katika mojawapo ya shule za msingi za jiji la Dar es Salaam, zaidi ya miaka 22 iliyopita, niliuona uwezo mkubwa wa uchambuzi ndani ya SHADRACK SAGATI, afisa wa habari katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji ambaye amefariki ghafla usiku wa Jumatatu (30-7-2018).

“Unastahili kuwa mwandishi wa habari. Kuna fursa nyingi za kujiendeleza katika uandishi wa habari. Jiandae, nitakusaidia kama utakuwa tayari ili uje usome katika chuo cha uandishi wa habari ninachofundisha,” nilimwambia Sagati.

Tulikuwa tumemaliza ibada ya Sabato, katika Kanisa la Waandventista wa Sabato la Magomeni Mwembechai ambapo yeye alikuwa akihudumu kama mwanakwaya katika kwaya ya Kanisa hilo.

Mwalimu Sagati alinisikiliza kwa makini na maneno yangu yalimwingia na kuuchoma moyo wake. Alitaka kujua ni namna gani ataweza kumudu kulipa ada na pia kazi yake ya ualimu wa shule ya msingi.

“All things are possible,” nilimwambia. Alishawishika palepale. Ndani ya muda mfupi alikuwa mwanafunzi wa cheti wa chuo cha uandishi wa habari cha Serikali (TSJ) na kuanza safari yake ya mafanikio makubwa katika fani ya uandishi wa habari hapa Tanzania.

Akiwa kijana mwenye akili nyingi, fikra pevu, mwenye bidii na hekima, Shadrack Sagati aliitumikia vema sana fani ya uandishi hadi kuwa mwandishi wa kutegemewa katika habari zinazohusu matukio makubwa ya kitaifa katika gazeti la Serikali la Habari Leo.

Wakati nikiwa nawakilisha taasisi Uingereza ya elimu ya biashara hapa nchini, The Association of Business Executives (ABE), Sagati alinipa ushirikiano wa hali ya juu sana. Nilizidi kugundua kuwa alikuwa mtiifu na pia hakusita kutoa ushauri wa kuboresha pale ilipobidi.

Siku moja nilimpigia simu kumpa habari. Wakati sakata la “the northen corridor”, pale “coalition of the willing”, wakiwa wamezimia kwenda bila Tanzania, nikatoa maoni yangu kuhusu ushirikiano mbadala wa Tanzania, Burundi, DRC na Comoro.

Aliandika habari katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la Habari Leo. Bungeni Marehemu Kepteni Komba na wabunge wenzake wakaibeba hoja hiyo na kulifanyia kazi.

Rais wa wakati huo, Mhe Dk Jakaya Kikwete aliona vema kwenda Bungeni na kwa hekima yake akalihitimisha suala hilo. Sagati alijaaliwa akili na wepesi wa kuchakata habari. Alijua habari nzuri iko wapi. Hakika aliendeleza kipaji cha ualimu katika fani ya habari.

Sagati hakuwa mwandishi wa kawaida. Alivuka viwango hivyo. Alikuwa mtu mwenye malengo makubwa. Kwanza alianza kwa kujiendeleza kielimu. Mbali na kurudi tena chuoni ili kuwa mahiri katika uandishi wa habari, Sagati alikwenda mbali zaidi na kupata Shahadi ya usimamizi wa biashara (Bachelor of Business Administration) katika chuo cha elimu ya biashara (CBE). Alianza masoma ya Shahada ya Uzamili.

Elimu ya biashara ilimsaidia kufanya tathmini nzuri na za kuvutia ambazo pia zilitumiwa na viongozi mbalimbali wa biashara na siasa. Wengi walimwita kwa ushauri na kuripoti habari zao kwa vile waliamini katika weledi wake na tunu zilizomuongoza katika maamuzi yake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: