Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha Nyamisatu kilichopo kata ya Mikumi mkoa wa Morogoro. Wa kwanza kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Hawa Mchafu Chakoma
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Hawa Mchafu Chakoma (wa kwanza kulia) akiuliza swali kwa watoa huduma kuhusu matumizi ya pamoja ya minara wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha Nyamisatu kilichopo kata ya Mikumi mkoani Morogoro. Aliyesimama katikati ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Mhandisi Albert Richard akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha Maharaka kilichopo kata ya Doma mkoani Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na wa pili kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Hawa Mchafu Chakoma.
Mlinzi wa mnara wa mawasiliano Bwana Shabani Mikidadi (wa kwanza kulia) akitoa taarifa kuhusu usalama na mazingira rafiki ya eneo la mnara huo kwa wajumbe wa Kamati ya Buge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha Nyamisatu kilichopo kata ya Mikumi, Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano akisikiliza
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu imezitaka kampuni za simu za mkononi kutumia ardhi inayomilikiwa na kijiji kujenga minara kwa ajili ya kufikisha mawasiliano kwenye maeneo mali mbali nchini
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kmati hiyo Mhe. Hawa Mchafu wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini wakiwa kwenye kijiji cha Mharaka kilichopo kwenye kata ya Doma mkoani Morogoro
Mhe. Mchafu amesema kuwa Kamati yake imebaini uwepo wa ujanja ujanja kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu ambao aidha wao wenyewe au kwa kupitia watu wao wa karibu wanaenda kwenye kijiji na kununua eneo ambalo kampuni imefanya tathmini na kuona kuwa linafaa kujenga minara na kumiliki eneo hilo.
Amefafanua kuwa watu hao wananunua maeneo hayo kwa kuwalaghai wananchi kuwa wanahitaji kuyamiliki ili waweze kuyaendeleza na baada ya muda mfupi eneo hilo linajengwa mnara wa mawasiliano ambapo anayemiliki analipwa na kampuni husika hivyo Serikali ya kijiji inakosa mapato.
Mhe. Mchafu Ameongeza kuwa utaratibu wa upatikanaji wa ardhi kwenye maeneo ya vijijini kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano hauko vizuri. Ameyataka makampuni ya simu yafuate utaratibu wa kujenga miundombinu ya mawasiliano ili wamiliki waliopo kwenye maeno hayo waweze kunufaika na uwekezaji huo. “Haiwezekani akawa ananufaika mtu mwingine wa kutoka Halmashauri nyingine na endapo jambo hili liionekana lina utata liletwe Bungeni kwa kuwa sisi ni chombo kinachotunga sheria ili wananchi wanufaike,” Mhe. Mchafu amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa anaishukuru Kamati kwa ziara hiyo na Serikali imepokea maelekezo. Nditiye ameuelekeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaotoa ruzuku kwa kampuni za simu ya kujenga minara hiyo kuhakikisha kuwa wanaweka masharti na vigezo kwenye nyaraka za zabuni ambazo wanapatiwa kampuni za simu kwa ajili ya kujenga minara kuwa wajenge minara kwenye ardhi inayomilikiwa na kijiji
Amefafanua kuwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu wanakuwa wajanja wanapata maeneo ambapo mnara wa mawasiliano utajengwa na kumilikiwa wao eneo hilo. “UCSAF wekeni vigezo na masharti kwenye zabuni na hakikisheni watoa huduma wamekagua eneo na liwe hilo lichukuliwe na kumilikiwa na Serikali ya kijiji ili kijiji kiweze kunufaika na kupata mapato”, Nditiye amesema. Ameongeza kuwa Serikali itasimamia na kufuatilia jambo hilo kwa kuwa inafanya kazi kwa karibu na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwatumikia wananchi na Wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa Wabunge ya kupatiwa mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali ya majimbo yao kwa niaba ya wananchi na Wizara inaipa UCSAF kuratibu na kutoa ruzuku kwa watoa huduma ili wajenge minara ya mawasiliano.
Naye mmoja wa wanakijiji wanaomiliki maeneo kwenye kijiji cha Maharaka kilichopo kata ya Doma mkoani Morogoro Bwana Arobogasti Theodore ameiambia Kamati hiyo kuwa aliuza eneo lake kwa mwalimu wa Sekondari ya Doma ambaye sio mkazi wa kijijini hapo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na baadae akaona mnara ukijengwa kwenye eneo hilo na mwalimu huyo kulipwa fedha za kukodisha eneo hilo kwa kampuni ya simu iliyojenga mnara mahali hapo.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mchafu amesema kuwa Serikali kupitia UCSAF na watoa huduma wanaojenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini ijiridhishe kabla ya kutoa ruzuku kuwa eneo linalojengwa mnara linamilikiwa na Serikali ya kijiji
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchafu ameyataka makampuni ya simu kutumia miundombinu kwa pamoja kwa ajili ya kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi badala ya kila mtoa huduma kujenga mnara wake peke yake
Naye Mhandisi Nditiye ameilekeza UCSAF kusimamia na kuhakikisha kuwa kampuni za simu zinatumia miundombinu kwa pamoja ili kufanikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi kwa kuwa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 inayataka makampuni ya simu yafanye hivyo. Pia, ameongeza kuwa kampuni ya Helios Tower tayari ipo na inajenga minara hiyo na kukodisha kwa kampuni za simu ili ziweze kutumia miundombinu hiyo kwa pamoja.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa taasisi yake itafuatilia na kusimamia utekelezaji wa sheria ya EPOCA kwa kuwa Serikali inaelekeza watoa huduma kujenga na kutumia minara ya mawasiliano kwa pamoja ili kupunguza gharama kwao za ujenzi wa minara hiyo ambapo baadae itaongeza gharama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
Toa Maoni Yako:
0 comments: