Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia) akimsikiliza mmiliki wa duka la vifaa vya ujenzi Wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati alipofanya ziara ya kikazi kujiridhidha utendaji kazi wa mashine za kielektroniki za Kutolea risiti (EFDs) ambazo mfumo wake ulipata hitilafu ya kiufundi hivi karibuni na kusababisha mashine hizo kutofanya kazi.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyevaa kofia) akikagua mashine ya kutolea risiti katika moja ya vituo vya mafuta Wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati alipofanya ziara ya kikazi kujiridhidha utendaji kazi wa mashine za kielektroniki za Kutolea risiti (EFDs) ambazo mfumo wake ulipata hitilafu ya kiufundi hivi karibuni na kusababisha mashine hizo kutofanya kazi.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyevaa kofia) akiwa ameongozana na Kaimu Meneja wa TRA, Bw. Deogratius Shuma (kushoto) pamoja na watendaji wengine wa Mamlaka wakielekea katika baadhi ya maduka Wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati kwa ajili ya kujiridhidha utendaji kazi wa mashine za kielektroniki za Kutolea risiti (EFDs) ambazo mfumo wake ulipata hitilafu ya kiufundi hivi karibuni na kusababisha mashine hizo kutofanya kazi. (PICHA ZOTE NA TRA).
Na Veronica Kazimoto, Kibaha.
Wafanyabiashara wamehimizwa kutumia Mashine za Kieletroniki za Kutolea Risiti (EFD) kwa kuwa mashine hizo kwa sasa zimeanza kufanya kazi na yeyote anayestahili kutumia mashine hiyo akiuza bidhaa au huduma bila kutoa risiti atatozwa faini ya shilingi milioni tatu hadi milioni nne na nusu.
Akizungumza mara baada ya kukagua mashine hizo leo wilayani Kibaha mkoani Pwani ambazo hivi karibuni mfumo wake ulipata hitilafu ya kiufundi na kusababisha baadhi ya mashine hizo kutokufanya kazi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amesema kuwa, wafanyabiashara wanatakiwa kutoa risiti kwa kila mauzo wanayoyafanya kwa sababu utoaji wa risiti hizo upo kwa mujibu wa sheria.
"Sasa hivi wafanyabiashara hawana kisingizio chochote kwa sababu mashine za EFD zote zinafanya kazi na mimi mwenyewe nimejiridhisha hivyo ni lazima kila mfanyabiashara anayestahili kutumia mashine ya EFD atoe risiti kila anapofanya mauzo na wananchi wanatakiwa kudai risiti kila wanaponunua bidhaa au huduma na kwa kufanya hivyo, Serikali itapata mapato yake stahiki," alisema Kichere.
Akizungumzia kwa upande adhabu ya kutokudai risiti, Kichere alisema kuwa, mwananchi yeyote akikamatwa amenunua bidhaa bila kuwa na risiti ya EFD atatozwa faini ya shilingi 30,000 hadi 1,500,000.
"Nawakumbusha wananchi wote kwamba, Suala hili la risiti linahusu pande zote mbili yaani mfanyabiashara na mnunuzi hivyo mtu akikiuka utoaji au upokeaji wa risiti atatozwa faini kama nilivyosema hapo awali," alisisitiza Kichere.
Naye mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi wilayani hapa Bw. Furaha Njabili amekiri kuwa, mashine hizo zinafanya kazi vizuri na amekuwa akitoa risiti kwa wananchi wanaonunua bidhaa dukani kwake bila matatizo yoyote.
Mnamo tarehe 11 Mei, 2018 Mfumo wa Kupokelea na Kuhudumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti ulipata hitilafu ya kiufundi na kusababisha baadhi ya mashine hizo kutokufanya kazi ambapo kwa sasa mfumo huo umetengemaa na mashine hizo za kielektroniki zimeanza kufanya kazi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: