Na Paul Mallimbo, Kampala.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (pichani)                   sssalikuwa mwanamapinduzi wa kweli, mzalendo na mzazi wa kila mtu akiwemo yeye Rais Museven.

Alisema kuwa kiongozi huyo wa kwanza wa taifa la Tanzania, alikuwa kiongozi pekee katika Bara la Afrika ambaye aliweza kuwaunganisha Watanzania wote pamoja na kuwa na makabila mengi na dini zao.

Rais Museven aliyasema hayo jana Juni mosi, wakati wa ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa Mwenyeheri na hatimaye kutangazwa mtakatifu, katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Watakatifu Mashahidi wa Uganda, jijini Kampala.

Alifafanua kuwa mchango wa Tanzania na Mwalimu Nyerere kwa Uganda, ulikuwa wa mazingira hatari sana katika kuhakikisha uongozi mbaya unaondolewa madarakani, mchango huo utakumbukwa daima.

"Kutokana na mchango huo, ni jukumu langu kuhakikisha siku hiyo inaadhimishwa kila Juni mosi hapa Uganda." Alisisitiza Rais Museven.

Alisema kuwa Uganda itaendelea kumkumbuka Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kwa mataifa ya mbali mbali ya Afrika ikiwemo ukombozi wa Uganda.

"Kwa kusali pamoja serikali na Kanisa Katoliki Uganda na Watanzania katika kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, tunaonyesha shukrani zetu za dhati kwa kiongozi huyo mkubwa wa aina yake, aliyewahi kutokea katika bara letu, alisema Rais Museven

Siku maalumu ya kumuombea Mwalimu Nyerere, ilianza rasmi Musoma, Mkoani Mara na baada ya hapo Serikali ya Uganda ilitenga kila siku ya Juni mosi kuwa siku maalumu ya ibada kwa ajili ya kuombea mchakato wa Baba wa Taifa kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu.

"Kama isingekuwa kujitoa kwa Mwalimu Nyerere kwa Uzalendo wake kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, Bara la Afrika lisingekuwa hapa lililopo leo,” Alisema.

Aliwaambia waumini waliohudhuria ibada hiyo kuwa Mama Nyerere anaendelea na kazi ambayo iliachwa na Baba wa Taifa ya kuwaunganisha wananchi kupitia siasa, ambapo yeye kwa sasa anaifanya kupitia kanisa.

Rais Museven ambaye amekuwa akihudhuria ibada ya kuombea mchakato huo, kama ahadi yake aliyoitoa miaka 12 iliyopita kuwa “Yeye mwenyewe atakapo kuwa na nafasi atahudhuria ibada hiyo”, alisisitiza kuwa ushirikiano ambao umejengwa na viongozi wa mataifa hayo mawili muda mrefu hapana budi kuenziwa kwa nguvu zote.

"Nina furaha kubwa kuwaona Watanzania wakija hija kila mwaka hapa nchini kwetu kuombea mchakato wa Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu unafanyika mapema zaidi,” alisema.

Akizungumza wakati wa ibada ya kuombea mchakato huo, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Kampala Dr. Cyprian Kizito Lwanga, aliwataka wakristu kumkumbuka Mungu ambaye amewapa watakatifu mashahidi wa Uganda ujasiri wa kumfia kristu.

Aliwataka pia wakristu kusali kupitia mashahidi hayo ili mchakato wa kumfanya Baba wa Taifa kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu uende kwa haraka.

Askofu Kizito alisema kuwa Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa na mtumishi wa Mungu ambaye anastahili kukumbukwa kwa sala kwa ajili ya mchakato wa kumfanya kuwa Mtakatifu. Alimshukuru Mama Maria Nyerere, wanahija kutoka Tanzania kwa upendo wao kwa Uganda na kwa Mashahidi wa Uganda.

Naye Mwakilishi wa Serikali ya Tanzania, kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, Bi. Mary Chiando, alimshukuru Rais Museven kwa kushiriki katika ibada hiyo na Askofu Cyprian Kizito kwa kuwapokea mahujaji kutoka Tanzania akisisitiza kuwa hiyo ni nafasi pekee ya kuwajua Mashahidi wa Uganda.

Naye Mwakilishi wa Familia ya Mama Nyerere, Sr. Eledina Ntandu alimwelezea Rais Museven kuwa ni kiongozi wa kweli wa Watanzania na Waganda na kwamba anatakiwa kuungwa mkono katika jitihada zake za kuleta maendeleo kwa wananchi.

Naye Padre Antonius Maria Mamsery ambaye pia alishiriki kuendesha ibada hiyo, alisema kuwa mwalimu Nyerere alizihudumia nchi zote za Afrika bila ubaguzi katika mapambano ya ukombozi wa nchi hizo. Aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyemwamini Mungu kiasi kwamba kila alipopatwa na changamoto katika uongozi wake alimshirikisha Mungu.

'Wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere hakupigania tu uhuru wa wanasiasa, bali pia alipigania ukombozi wa Wakristu, kila Mtanzania na Afrika kwa ujumla,” Alifafanua.

Mama Maria Nyerere pamoja na familia yake, wakishirikiana na maelfu ya Watanzania, wako nchini Uganda katika jiji la Kampala kwa ajili ya hija pamoja na ibada ya kuombea mchakato wa baba wa Taifa mwalimu Nyerere kuwa mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu.

Ibada ya kuombea mchakato wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu ulianza miaka 12 iliyopita, na utaendelea mpaka hapo kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani atakapomtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu. Mwisho.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: