Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) amekabidhi hundi ya shilingi Milioni 6.8 ( 6,830,000/=) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika zahanati ya kijiji cha Solwa kilichopo kata ya Solwa jimbo la Solwa mkoani Shinyanga.
Akizungumza leo wakati wa kukabidhi hundi hiyo kwa kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo,Mheshimiwa Azza alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa alipotembelea zanahati hiyo mwezi Mei mwaka huu na kukuta changamoto ya uhaba wa vyumba vya kutolea huduma za afya ikiwemo wodi ya watoto na akina mama.
“Nilifanya ziara katika zanahati hii mwezi Mei mwaka huu wakati natoa vitanda vya kujifungulia na viti vya wagonjwa,baada ya kuingia katika chumba cha akina mama nilikuta vitanda vitatu,niliguswa na jinsi akina mama walivyokuwa wanahangaika,lakini nikaambiwa wananchi wana mpango wa kujenga wodi ya watoto na akina mama,nikaahidi kuchangia mabati 20 pindi majengo yatakapofikia hatua ya upauaji”,alieleza mbunge huyo.
“Mwezi Septemba mwaka huu,Diwani wa kata ya Solwa alinitumia picha za majengo mawili yakiwa tayari kwa upauaji,nikawaza kuhusu mabati yangu 20,nikaona hayatoshi,ndipo nikaamua kuanza kutafuta watu wa kunisaidia,juzi nikapokea ujumbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kuwa wamekubali ombi langu na wameamua kutoa shilingi 6,830,000/= kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo moja”,alieleza mheshimiwa Azza Hilal Hamad.
Toa Maoni Yako:
0 comments: