Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza wahifadhi wote nchini kushirikiana na wadau wengine hasa mamlaka za Mikoa na Wilaya katika maeneo yenye uvamizi wa mifugo na migogoro ya mipaka ya hifadhi ili kutatua changamoto hizo kwa namna shirikishi ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.
Ametoa agizo hilo Disemba, 16, 2017 katika Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wakati akifunga mafunzo ya 15 ya mabadiliko ya kuelekea mfumo wa Jeshi Usu kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
“Kazi ya ulinzi wa rasilimali zetu za asili ni yetu na tutaiendeleza, Falsafa yetu ni kuwashirikisha wadau wote, kama kuna taasisi za kiraia kwenye eneo lako la kazi, taasisi za kijamii, mamlaka za mikoa na wilaya, wananchi, halmashauri husika mshirikiane nao ili kupunguza madhara ya operesheni zetu, na zoezi hili la uhifadhi liwe endelevu,” alisema Dk. Kigwangalla.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuheshimu Sheria za nchi na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo kuingiza mifugo, kuanzisha kilimo, makazi na ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na matumizi mengineyo.
Awali akizungumzia mafunzo hayo alisema, lengo ni kubadilisha utendaji katika sekta ya uhifadhi kutoka ule wa kiraia kwenda wa jeshi usu ambao utaongeza nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na maadili kwa watumishi wote wa sekta hiyo ili waweze kusimamia ipasavyo uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: