Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na badhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera alipowasili katika Ofisi hiyo ili kuzungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera kuhusu masuala ya kiutendaji alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani humo.
Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Kagera, Bw. Adam Ntoga, akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani Kagera.
Baadhi ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumzia kuhusu uadilifu katika kazi na utoaji wa elimu kwa mlipakodi baada ya Naibu Waziri huyo kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera, alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo ambapo amewaasa kuwa waadilifu katika kazi zao.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati -walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera na baadhi ya Maafisa Waandamizi katika Mkoa huo.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Kagera Bw. Seif Mkude (kulia) akielezea kuhusu utayari wa wafanyabiashara wa Mkoa huo kulipa kodi wakati wa Mkutano kati ya wafanyabiashara wa Mkoa huo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati).
Mfanyabiashara wa Mkoa wa Kagera Bw. Taimur Manyilizo, akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafanyabiashara Mkoani humo ikiwemo kile alichoeleza uwepo wa taasisi nyingi zinazodai kodi nyingi ikiwemo OSHA, TFDA, Zimamoto ambapo aliiomba Serikali iziangalie na kuzifanyia kazi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera katika kukuza Uchumi wa nchi baada ya Naibu Waziri huyo kufanyaziara ya kikazi Mkoani humo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - WFM).
Serikali imelipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.
Hayo yamesemwa Mjini Bukoba mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dokta Ashatu Kijaji (Mb), wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa huo akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Dokta Kijaji alisema kuwa wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Shilingi bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai wengine wakilipwa shilingi bilioni 24.
Alisema kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa madeni yote yaliyohakikiwa.
Dkt. Kijaji aliiambia Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera kwamba Serikali inatambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao, kutoa stakabadhi wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai stakabadhi wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi hizo zinaonesha kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.
Akizungumza kwaniaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Seif Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.
Alisema kuwa wafanyabiashara wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa kikamilifu na kutekeleza miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea kulipa kodi hizo ili kujenga uchumi wa nchi.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli huku akiishauri Serikali kuondoa kero ndogondogo zilizotolewa na wafanyabiashara wakati wa mkutano huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro, aliwashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.
Alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara hao kusafirisha bidhaa zaidi nje ya nchi ili kuvutia fedha za kigeni.
Toa Maoni Yako:
0 comments: