Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina (wa tatu kushoto), wakati alipokagua daraja la Kinambo lililopo katika barabara ya Kasansa-Muze KM 31.90 wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
 Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina (wa tatu kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa fulana nyeusi), wakati alipokagua daraja la Kinambo lililopo katika barabara ya Kasansa-Muze KM 31.90 wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
 Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa daraja la Kinambo lililopo katika barabara ya Kasansa-Muze KM 31.90 wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
 Muonekano wa mitambo ya kuchimbia nguzo za Daraja la Mto Momba unaounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Groups) Corporation, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mto Momba linalounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe.
 Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati wa mkutano na wananchi wa Kilymatundu mara baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mto Momba, wilayani Sumbawanga.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Kilymatundu mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mto Momba, wilayani Sumbawanga.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Kilyamatundu kilichopo wilayani Sumbawanga akimkabidhi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ushahidi wa picha za miti iliyokatwa katika shamba lake kupisha mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto Momba, mkoani Rukwa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Imeelezwa kuwa kukamilika kwa Daraja la Mto Momba linalounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe kutafufua fursa za kiuchumi katika mikoa ya magharibi na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo leo alipokagua ujenzi wa daraja hilo na kuwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha daraja hilo linakamilika mwezi Agosti mwakani.

“Toeni ushirikiano unaostahili kwa mkandarasi ili Daraja hili la Momba na madaraja madogo saba yanayojengwa katika barabara ya Kasansa-Kilyamatundu yenye urefu wa KM 210.38 yakamilike kwa wakati”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesisitiza nia ya Serikali ya kujenga barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 na Stalike-Kilyamatundu-Mloo KM 500 kwa kiwango cha lami ili kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa mazao ya kilimo na mifugo katika Bonde la Mto Rukwa kwenda maeneo mingine ya nchi.

“Wale wote ambao wamewekewa alama za kubomoa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara nawaomba wafanye hivyo mapema ili kuwawezesha wakandarasi kufanya kazi zao kwa uhuru na kuiwezesha TANROADS kufanya usanifu wa kina”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina, amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa watamsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga Daraja la Momba na madaraja madogo saba katika barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 ili kazi ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha, amewataka wananchi watakaopata fursa za ujenzi wa madaraja hayo kuepuka vitendo vya wizi na hujuma kwa wakandarasi.

Amesema kukamilika kwa Daraja la Momba kuna manufaa mengi kiuchumi, kijamii kwa kuwa daraja hilo litawaunganisha wakazi wa jimbo lake na mkoa wa Songwe na hivyo kuharakisha shughuli za kimaendeleo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: