Upepo umebadilika katika kesi baina ya Tigo Tanzania na wasanii maarufu wa mziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinyikuma maarufu MwanaFA na Ambwene Yesaya maarufu AY, baada ya Mahakama Wilaya ya Ilala kutupilia mbali pingamizi la awali lililowekwa na wasanii hao.
Mahakama hiyo sasa imekubali kusikiliza maombi ya Kampuni ya Tigo kuhusu kujumuishwa kwa kampuni ya Cellular Tanzania Limited kwenye hukumu kama mmoja wa wadaiwa wa fidia ya Sh 2.1 bilioni. Hapo awali Mahakama ilikuwa imeamuru kampuni ya Tigo kuwalipa wasanii hao kwa madai ya kutumia nyimbo zao zenye hati miliki bila ruksa.
Pia Mahakama imekubali kusikiliza ombi la Tigo la kurekebishwa makosa ya kiuandishi yanayohusu majina ya wahusika katika kesi hiyo, ambapo jina la Hamis Mwinjuma ndilo liloandikwa kwenye hukumu wakati Hamis Mwinyijuma ndilo jina linaloonekana kwenye hati ya madai. Vilevile hukumu inaonesha jina Ambwene Yessayah wakati jina lililopo kwenye hati ya madai ni Ambwene Yesaya.
Vile vile, kampuni ya Cellular Tanzania Limited ambayo Tigo inadai ndio ilioingia nayo mkataba wa kutoa huduma za muziki haikuwa imejumuishwa kwenye hukumu hiyo. Hapo awali, kampuni hiyo ya Ms Cellular Tanzania ilikuwa imeandikia barua Mahakama ikibainisha kuwa ndiyo iliyokuwa imeisambazia kampuni ya Tigo nyimbo hizo. Katika barua yenyewe, Cellular Tanzania ilidai kuwa ilinunua nyimbo hizo za Usije Mjini wa MwanaFA na Dakika moja wa AYkutoka kwa kampuni ya Sony Music Entertainment Africa Limited ambayo walikuwa na mkataba na watayarishaji wa nyimbo hizo.
Wasanii hao kupitia wakili Albert Msando waliweka pingamizi kuhusu maombi ya Tigo, wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali. Walidai kifungu cha 96 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai kilichotumika kufungua maombi hakiiwezeshi Mahakama kutekeleza maombi hayo kwa sababu kosa la kutoihusisha kampuni hiyo ya Cellular Tanzania siyo la kiuandishi wa hesabu.
Akitoa uamuzi wa Mahakama, Hakimu Mfawidhi, Ritha Tarimo alisema hoja za wasanii hao hazipaswi kuwasilishwa kama pingamizi, hivyo alipanga kusikiliza maombi hayo Oktoba 18.
Awali, Tigo ilifungua maombi Mahakama Kuu ikiomba kusimamishwa utekelazaji wa hukumu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: