ABE, bodi inayotoa kozi mbalimbali kutoka nchini Uingereza, yaandaa
hafla fupi iliyowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya elimu
nchini Tanzania na matokeo yake katika ajira kwa vijana. Hafla hiyo
ilishirikisha watu wenye taaluma mbalimbali kama vile watoa elimu,
wanafunzi, makampuni ya ajira, maafisa wa rasilimali watu, wafanyakazi
wa makampuni binafsi na serikalini, vyombo vya habari na wananchi
wengine wanaoguswa na tatizo hilo.
Katika hafla hiyo,
jopo lililoteuliwa na waandaji liliongoza majadiliano yaliyowapa
changamoto wadau kutafuta njia za kupunguza tatizo la idadi kubwa ya
wanafunzi wanaomaliza masomo kila mwaka ambao wanakosa nafasi za ajira.
Majadiliano hayo yalitoa hamasa kwa wadau kubainisha ujuzi na vigezo
vinavyohitajika zaidi na waajiri na namna ya kuwasaidia wahitimu kupata
ujuzi huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa ABE nchini Tanzania, Bi
Zaituni Ituja alisema, “Wote tunafahamu kuwa wahitimu wengi hawana
ajira. Lakini pia tunasikia makampuni yanalalamika kuwa hawapati vijana
wa kuwaajiri wenye vigezo. Je, tatizo ni kuwa makampuni hayajui pa
kutafuta wafanyakazi au wanapata vijana wasiokidhi vigezo? Swali hili
ndio chanzo kikubwa cha sisi kuandaa hafla hii na tunatarajia wadau
wataona umuhimu wa kuendeleza mjadala huu na kufanyia kazi mapendekezo
haya.”
Mbali na majadiliano hayo, wageni walipata
muda wa kufahamiana baina ya waalikwa kupitia zoezi la utambulisho
lililoongozwa na mwendeshaji wa hafla hiyo. Waalikwa walipata fursa ya
kubadilishana mawasiliano ya kibishara kwa lengo la kujenga mahusiano
kama ilivyokuwa dhamira ya hafla hiyo katika kuwakutanisha wadau wa
elimu na ajira Tanzania.
ABE inafanya shughuli zake kwa zaidi ya miaka 40 katika nchi zaidi ya 100 duniani na imewekeza katika kuhakikisha inatoa kiwango cha elimu cha hali ya juu. Kozi zinazotolewa ni kozi za masomo ya biashara ambazo zinaweza kumsaidia mtu kupata shahada ya chuo au kumwezesha mtu kupanda cheo. ABE inatoa kozi za Business Management, Business Start-up and Entrepreneurship, Human Resource Management, Marketing Management na Travel, Tourism and Hospitality Management.
Kozi hizi zinaweza kusomwa na watu ambao wako kwenye ajira na wanataka tu kukuza uwezo wao na kupanda cheo, au wanaotaka kutumia ABE kama njia ya kupata nafasi ya kujiunga na vyuo mbalimbali duniani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: