WATU zaidi ya 50 wamenusurika kufa mara baada ya kitu kinachosadikiwa kuwa bomu lililotengenezwa kwa mkono kulipuka na kuwajeruhi vibaya watu 15 sehem mbalimbali za mwili katika bar ya Arusha Night Park iliyopo maeneo ya Mianzini mjini hapa.

Watu hao walijeruhiwa vibaya na mlipuko huo mapema jana, april 13 majira 1;30 jioni mara baada ya watu hao waliokuwa wakipumzika katika baa hiyo kwa lengo la kuangalia mpira kukusanyika.

Akizungumza baada ya kutembea eneo la tukio na kutembelea majeruhi hao katika hospitali ya Selian, na Mount Meru mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema kuwa tukio hilo limetokea bila kuwepo kwa mitazamio yeyote hivyo kuwataka wananchi wawache vyombo vya dola kufanya kazi yao ya uchunguzi.

Mulongo alieleza kuwa katika tukio hilo watu walikuwa wanaendelea na kazi zao na ndipo mara waliposikia kitu kama kishindo na ghafla ndipo watu hao walipoanza kurupushani za hapa na pale kutokana na mlipuko huo wa bom.

Alisema kuwa, baada ya tukio hilo polisi walifika eneo la tukio na kuwachukua majeruhi hao na kuwapelekea katika hospitali ya Mount Meru, Selian, na hospitali ya st.elizabeth, pamoja na mount meru kwa ajili ya kupata matibabu.

Aidha kati ya majeruhi hao 15, watatu walitibiwa na kuruhusiwa ambapo 12 wanaendelea na matibabu huku wawili kati yao akiwa na majeraha makubwa kwenye miguu ambaye alikuwa karibu na eneo bomu lililopotegeshewa .

Aidha Mkuu wa mkoa wa Arusha alitoa rai kwa watanzania kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pale wanapokuwa na taarifa za mtu yeyote kuhusika na tukio hilo hali ambayo imekuwa ikitishia amani kutokana na tukio hilo kujirudia rudia.

Mulongo alisema kuwa uchunguzi zaidi unaendelea kupitia kamera zilizokuwa zimefungwa kwenye bar hiyo katika kuwatambua wale wote waliohusika na tukio ambapo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Mount Meru, mhudumu Luis John alisema kuwa, alishtukia kishindo na moshi mkubwa wakati akihudumia wateja na watu kukimbia bila mwelekeo.

Aidha alisema kuwa , bomu hilo linaonekana lilikuwa limetegwa ndani ya bar hiyo ambapo asilimia kubwa ya wateja walikuwa wakiangalia mpira na ndio wengi wao waliojeruhiwa kutokana na bomu hilo ambapo walianza kukimbia kimbia.

Alisema kuwa hasara waliyoipata baada ya mlipuko huo ni baadhi ya wateja walikuwa wameshahudumiwa walikimbia na bili huku wengine wakipoteza simu zao.

Wahudumu  wengine wa bar hiyo waliojeruhiwa ni Suzan John, Joyce William, na Meneja wa bar hiyo aliyetambulika kwa jina la Halima .

Hata hivyo hivyo baadhi wa wananchi wakizungumzia tukio hilo walisema kuwa matukio ya kulipuka kwa mabomu mkoani Arusha yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kusababisha kuwepo kwa hofu kubwa miongoni mwa wananchi hasa ikizingatiwa mengi yao kupigwa sehem zenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Mwananachi huyo aliyejitambulisha kwa jina la ,Ashura Salimu mkazi Soweto alisema kuwa, matukio hayo yamekuwa yakiwafanya kuishi kwa wasiwasi mkubwa ,kwani yamekuwa yakijirudia mara kwa mara huku viongozi wa mkoa na Rais Kiwete wakitoa matamko ya kuwasaka hadi kuwapata na kuwachukulia hatua za kisheria lakini matokeo yake huishia hewani.

“Kama unavyotambua hili si tukio la kwanza kutokea hapa Arusha, yametokea mabom mengi tu ikiwemo la uwanjani hapa Soweto na lile la kanisani lililigharimu maisha ya watu ambapo mbali na serikali ya mkoa kufika na kulitokea tamko lakini pia Rais Kikwete alitoa tamko la kuwasaka na kuhakikisha wanapatikana na kuchukuliwa hatua lakini kwa matokeo yake walitupa taarifa kuwa wahusika wamewapata na wanawajua hivyo watawachukulia hatua kali za kisheria, lakini maneno hayo baadae yalikuja kuonekena na kuungwa ungwa kutokana na watu hao hawakutajwa majina kwa madai kuharibu upelelezi lakini pia hatuwajui hadi leo na hakuna hatua waliochukuliwa”

Hivyo aliomba serikali kuhakikisha kuwa inakuwa makini na kuchukua hatua za haraka kwa watu hao ambao wamekuwa wakihusika na matukio hayo kwani kwa mkoa wa Arusha imekuwa ikizua wasiwasi mkubwa badala ya kuunga unga maneno wakati matukio hayo yanagharimu maisha ya watanzania.

Aidha itakumbukwa kuwa hili ni bomu la nne kurushwa kwenye mikusanyiko ya watu ambapo bomu la kwanza lilirushwa katika kanisa la katoliki la Joseph Mfanyakazi liilopo olasiti katika uzinduzi wa kanisa hilo, huku tukio la pili lilirushwa katika viwanja vya Soweto katika mkutano wa kufunga kampeni za chadema , na la tatu likirushwa katika mkesha wa mwaka mpya katika kanisa katoliki usa river .
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: