Wazungu wakishow love na babu kwa mshangao zaidi.

Mama wa kihindi akimsalimia kwa heshima Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile.

---
Na Mwandishi Wetu, Loliondo

Tiba ya kikombe inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile ni balaa, mvuto wake unaitikisa dunia na hivi sasa Wahindi na Wazungu wamejaa Kijiji cha Samunge, Loliondo kupata huduma hiyo.

Uchunguzi wa uliofanywa umebaini kuwa, Wazungu, Wahindi na raia wengine wa kigeni wanaendelea kumiminika Loliondo kutokana na ripoti wanazopata.

Pia imebainika kuwa, vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vimekuwa vikiripoti kuhusu miujiza ya Babu wa Loliondo, hivyo kutoa hamasa kwa watu wa mataifa kuja nchini kupata kikombe cha tiba.

Wiki iliyopita, Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani ya Radio Deutsche Welle (DW) ambayo husikika dunia nzima, ilitoa makala maalum inayoelezea tiba ya Babu Ambi wa Loliondo.

Mbali na DW, mashirika mengine ya habari ya kimataifa ambayo kwa nyakati tofauti yamekuwa yakiripoti kuhusu miujiza ya Babu ni BBC na VOA, zote kupitia idhaa zake za Kiswahili.

Vyombo hivyo vya habari vimeupaisha umaarufu wa Babu kiasi cha raia wengi wa kigeni kutamani kufika kumuona kwa macho ‘mganga’ huyo aliyedai kuoteshwa dawa hiyo na Mungu.

Uchunguzi unaonesha kwamba, mpaka sasa raia zaidi ya 3,000 wa kigeni wameshafika kwa Babu na kupata kikombe cha dawa huku wengine wakiwa wanaulizia njia ya kufika wakiwa jijini Arusha.

Mpaka sasa watu 70 kutoka barani Ulaya wameshapata kikombe cha Babu, wakati Wahindi wameendelea kuzagaa Samunge utadhani ndipo yalipo makazi yao ya siku zote.

Kwa muda mrefu sasa, Wahindi wamekuwa wengi Loliondo tangu tiba hiyo ya miujiza ilipopata umaarufu mwishoni mwa Februari, mwaka huu huku baadhi yao wakitoa huduma kama wasaidizi wa mzee huyo.

Takwimu zilizokusanywa katika eneo la utoaji wa dawa zinaonesha kuwa, wageni kutoka nchi jirani ya Kenya ndiyo wanaoongoza kwa kunywa dawa hiyo.
Mpaka sasa, zaidi ya Wakenya 2,400 wameripotiwa kupata kikombe cha Babu.

Nchi nyingine ambazo raia wake wameshafika kijijini Samunge na kunywa dawa hiyo ni Marekani, Finland, Uholanzi, Siri Lanka, Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE), Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Uganda, Rwanda, Burundi na Comoro.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

1 comments: