Kesho ni siku ya Mashujaa Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein atawaongoza wananchi katika kumbukumbu ya mashujaa Mjini Zanzibar.

Kesho kutasomwa hitma katika Afisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi Kisiwandui Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu mzee Abeid Amani Karume.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atahudhuria shughuli ya kisomo hapo kesho Zanzibar pamoja na Viongozi wengine na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

Shughuli za kisomo cha hitma zimepangwa kuanza saa 3:00 asubuhi na kufikia tamati saa 6:00 mchana. Mbali na shughuli za kisomo,pia viongozi wataweka shada la maua kaburini.

Itakumbukwa kuwa tarehe kama ya kesho (07/04/1972) ndio siku ambayo Rais wa kwanza wa Zanzibar na Makamu wa kwanza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa kwa kupigwa risasi nane na wapinga maendeleo alipokuwa Makao Makuu ya Chama cha Afro Shiraz(ASP) Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Mzee Karume aliuwawa siku ya Ijumaa saa 12.05 jioni alipokuwa amekaa katika ukumbi chini wa Jengo la ASP na wazee wengine wa Chama (ASP).

Katika ukumbi huo kulikuwa na meza moja iliyozungukwa na viti sita ambayo wakuu hao walikaa, katika viti vitatu vilivyoelekea upande wa kusini, cha kwanza upande wa magharibi mkabala na mlango wa nje wa kuingilia, ndicho alichokaa marehemu marehemu Mzee Karume.

Kiti cha pili alikaa Mstahiki Meya wa Mji wa Zanzibar, na Makamu wa Rais wa ASP, Mtoro Rehani Kingo ambaye aliondoka kwa muda mfupi kwenda msalani.

Kiti cha tatu alikaa Muhidini Ali Omar, mzee mashuhuri wa ASP na Mbunge, viti vilivyoelekea Kaskazini cha kwanza alikaa Shaha Kombo, Mshika Fedha wa ASP na Mbunge akielekezana na Mzee Karume, kiti cha pili alikaaThabit Kombo Jecha Katibu Mkuu wa ASP na Mwenyekiti (Waziri) Biashara na Viwanda na kiti cha mwisho alikaa Ibrahim Sadalla mzee mwengine mashuhuri wa Chama hicho.

Wakati huo, Mzee Karume alikuwa katika mazungumzo ya kawaida na wazee wenziwe na kumsubiri Mzee Mtoro Reheni Kingo arejee wacheze Dama na mchezo wa dhumna.

Wauaji walitumia silaha aina ya “Automatic Sub-mashine Gun” zenye kaliba ya 7.62 mm. baada ya kupigwa risasi, Mzee Karume alikimbizwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake kwa muda wa dakika 45,lakini hawakufaulu.

Marehemu Mzee Karume amezikwa siku ya Jumatatu tarehe 10/04/1972 Makao Makuu ya ASP Kisiwandui Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja saa 6:00 mchana.

IMETOLEWA NA;
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
TAREHE 06/04/2011
ZANZIBAR, TANZANIA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: