Amani, Heshima na Upendo kwako.
Kwanza napenda kumshukuru MUNGU kwa uhai wa kila mmoja wetu. Ni uhai huo unaotufanya sasa kuwasiliana hivi.
Pili napenda kutoa shukrani kwa kazi kubwa unayoifanya katika KUIELIMISHA, KUIBURUDISHA NA / AMA KUIKOMBOA JAMII YETU YA TANZANIA ambayo kwa hakika yatuhitaji sote. Tumekuwa pamoja katika kutimiza hili na najivunia uwingi wa blog zetu na utofauti wa maudhui yetu unaowafanya watu tofauti wenye kusaka "ladha" tofauti za habari-na-matukio kupata vyote toka kwetu.
Na sasa mwaka 2009 unakwisha na tunaelekea kuanza mwaka mpya wa 2010. Nakutakia mafanikio katika kila jema utendalo na hasa katika WAJIBU WETU WA HIARI wa kuisaidia jamii yetu ya Tanzania.
Lakini tunapoanza mwaka mpya, kuna mambo mawili ambayo ningependa kuomba na kusisitiza ndani ya jamii yetu.
Kwanza ni USHIRIKIANO. Tumeona ongezeko la wanajamii kwenye ulimwengu wa ku-blog na hili ni jambo jema. Lakini lina wema kama tutaweza kuungana na kuonesha UMUHIMU wa uwepo wetu. Tuko katika nyanja ama maudhui mbalimbali kama vile taswira, habari, uchambuzi, utambuzi, mitindo, mitazamo, imani nk, lakini sote twafanya haya kuiinua jami yetu ya Tanzania. Tunahitaji kuunganisha nguvu kwa kusomana, kutoleana maoni ambayo yanasisitiza, yanakosoa na kuelimisha zaidi jamii yetu.
Pili ni KUIREJESHEA JAMII. Kama sote twaandika kwa ajili ya jamii, basi tuwaze "ni kipi tutakachoifanyia jamii yetu kwa mwaka ujao kuionesha kuwa tuko pamoja nayo?" Binafsi niliwaza kuwa baada ya kumalizika kwa KONGAMANO LA BLOGGERS mwezi Februari, tuangalie namna ya kuunganisha nguvu na kufanya jambo moja la kuwajali walio katika mazingira magumu katika kuadhimisha SIKU YA KU-BLOG DUNIANI.
Naamini tukianza mapema kukusanya michango kidogokidogo (hata kwa kutumia kamati itakayoaminika baada ya kongamano) tunaweza kufikia kiasi cha kubadili maisha ya jamii mojawapo. Iwe ni kuwanunulia mahitaji muhimu yatima ama kununua madawati, kujenga darasa, kusaidia maabara ama lolote litakaloonesha kuwa nasi tumetoka kwenye jamii hiyo, tunaikumbuka na tuko nayo katika kusaidia kutatua matatizo wanayokabiliana nayo.
Tumeona mifano ya ndugu zetu waliounganisha nguvu na kufanikiwa kuibadili jamii (mfano ni hawa TUWA-USA http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/11/tuwa-usamashujaa-wetu.html)
Haya ni mawazo ambayo naomba yawe kama chachu ya kujua nini twaweza kufanya kwa UMOJA kama wana-blog na kuirejeshea jamii.
Nawapenda nyote, nawaheshimu na nawaombea pia
Kwa niaba ya familia yangu na wana-changamoto wote, NAWATAKIA KILA LILILO JEMA KATIKA KUMALIZA MWAKA HUU NA KUANZA UJAO
BLESSINGS
Toa Maoni Yako:
0 comments: