
Mtu mmoja amepewa kifungo cha maisha gerezani huku wengine wakifungwa kwa vipindi vya hadi miaka 15 kwa kuhusika na mauaji ya Albino 12 ambao viungo vya miili yao iliuzwa kwa wachawi.
Mahakama ya mkoani Ruyigi pia iliwaachilia huru washukiwa wengine watatu kwa kutopatikana na hatia.
Albino hao waliuawa, miili yao ikakatwakatwa na viungo vyao vikauzwa nchini Tanzania ambako zaidi ya Albino 40 wameuawa katika kipindi cha mwaka mmoja.
Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakiongozeka tangu mwaka wa 2007 kutokana na imani za kishirikina kwamba viungo vyao kama vile nywele, viganja, miguu na sehemu za siri zaweza kumletea mteja ufanisi katika mapenzi, biashara na maisha kwa jumla.
Ingawa visa vingi vya mauaji ya Albino vimeripotiwa Tanzania ambako zaidi ya washukiwa 200 wamekamatwa, hakuna yeyote ambaye amehukumiwa.
Kutokana na uamuzi wa mahakama ya Burundi, shirika moja la kutetea haki za Albino nchini humo, limeelezea kuridhika kwake na hatua hiyo lakini likatoa wito kwa serikali kuongeza jitihada ili kukomesha uhalifu huo.


Toa Maoni Yako:
0 comments: