RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume, akizungumza na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Marekani Pamela White, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar Kumuaga Rais, baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.

PICHA NA RAMADHAN OTHMAN IKULU

*Shirika la Misaada la Marekani USAID laipongeza Serikali ya Zanzibar

MKURUGENZI Mkazi wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani USAID, Bi Pamela White amepongeza hatua za maendeleo zilizopatikana hapa Zanzibar na kueleza kuwa Shirika hilo litaendelea kuunga mkono hatua hizo kwa lengo la kupata mafanikio zaidi.

Pamela White ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga kutokana na kumaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania, alieleza hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Amani Abeid Karume.

Katika mazungumzo hayo, White alimueleza Rais Karume kuwa katika kipindi chake chote alichofanya kazi nchini Tanzania ameweza kugundua maendeleo ya haraka haraka yaliopatikana Zanzibar kutokana na kuimarishwa kwa sekta za maendeleo zikiwemo sekta za afya na elimu.

Akitoa shukurani zake yeye mwenyewe binafsi na kwa niaba ya Shirika la USAID, White alimueleza Rais Karume kuwa kitendo cha kupiga vita Malaria kimeweza kuleta mafanikio makubwa hapa Zanzibar na kitaendelea kuijengea sifa duniani kote sambamba na kupanua wigo kwa nchi nyengine ambazo zimo katika mapambano hayo.

Alieza kuwa mafanikio hayo yameweza kuiweka Zanzibar katika mfano mzuri wa kuigwa na Mataifa mbali mbali duniani katika kupiga vita maradhi hayo ambayo yamekuwa yakizisumbua nchi nyingi zikiwemo nchi zinazoendelea.

“ Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na yote hayo yanatokanana uongozi mzuri uliopo madarakani, na USAID imevutiwa sana na mafanikio hayo,”alisema White.

Aidha, Mkurugenzi huyo, alimueleza Rais Karume kuwa mbali ya mafanikio yaliopatikana katika sekta ya afya pia mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika sekta ya Elimu.
Alieleza kuwa sekta ya elimu imeweza kupiga hatua kwa kiasi kikubwa hali ambayo imeza kuwavutia Washirika wa Maendeleo likiwemo Shirika la USAID kuendelea kuiunga mkono sekta hiyo kutokana na mafanikio yaliopatikana.

White anaehamishiwa nchini Liberia baada ya kufanyakazi nchini kwa kiaka minne, alimueleza Rais Karume kuwa anajivunia mashirikiano mazuri aliyoyapata katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara na Taasisi mbali mbali kupitia viongozi wake ambao walimpa ushirikiano wa kutosha hali ambayo ilimrahisishia kufanya kazi zake wakati wote.

Sambamba na hayo, White alimueleza Rais Karume kuwa yeye mwenyewe binafsi amevutiwa na mazingira ya visiwa vya Zanzibar kutokana na vivutio vingi vya kitalii, mipango iliyowekwa katika kuinua sekta hiyo ikiwemo uimarishwaji wa miundombinu ya barabara hali ambayo imepelekea Zanzibar kupiga hatua katika sekta hiyo.

Nae Rais Karume alitoa pongezi zake kwa Mkurugunzi huyo kutokana na mashirikiano mazuri aliyoyatoa katika kusukuma gurudumu la maenmdeleo hapa Zanzibar kutokana na misaada yake mbali mbali iliyotolewa na Shirika la USAID katika kuinua sekta za maendeleo na uchumi.

Dk. Karume alimueleza Bi White kuwa Zanzibar inathamini sana mashirikiano sambamba na misaada inayopata kutoka Shirika la USAID hatua ambazo zimeweza kutumiwa vizuri katika kuimarisha sekta za maendeleo na hatimae kuweza kuleta mafanikio.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa, amepata faraja kwa kumsikia yeye mwenye binafsi jinsi anavyoeleza mafanikio yaliopatikana Zanzibar katika sekta za maendeleo hali ambayo changamoto kwa Zanzibar kuelendelea na juhudi zake za kujiletea maendeleo endelevu.

Rais Karume alisema kuwa hatua kubwa zimeshafikiwa na Zanzibar katika kuziimarisha sekta za maendeleo zikiwemo elimu, afya, mawasiliano, miundombinu ya barabara, huduma ya maji safi na salama na sekta nyenginezo ambapo kwa hivi sasa kazi kubwa inayofanyika ni kuziimarisha zaidi sekta hizo ili ziendelee kuleta maendeleo sambamba na kuchangia kukuza uchumi.

Aidha, Rais Karume alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa mafanikio yalipatikana Zanzibar katika kupiga vita Malaria yameweza kupatikana kutokana na mashirikiano mazuri zaidi yaliopo kati ya Zanzibar na Shirika la USAID.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Mohammed Jidawi nae alitoa shukurani zake kwa Shirika hilo na kueleza kuwa mbali ya msaada wa kupiga vita malaria uliotolewa na USAID pia limeweza kuisaidia Wizara ya Afya katika kutoa elimu ya afya, uzazi wa mpango, kutoa vifaa katika kitengo cha elimu ya afya, majengo na misaada mnyengineyo.

Habari na Picha kwa Hisani ya Rajab Mkasaba wa Ikulu Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: