ZAIN, kampuni ya simu inayotoa huduma katika nchi 22 Mashariki ya Kati na Afrika, imepanua wigo wa huduma yake ya One Network katika nchi ya Saudi Arabia, Mashariki ya Kati, ikiwa ni moja ya hatua kubwa zilizopigwa na kampuni hiyo.Meneja Masoko wa Zain Tanzania, Costantine Magavilla alisema Dar es Salaam kwamba Zain ilianza kutoa huduma hiyo katika Ufalme wa Saudi Arabia wikiendi iliyopita na papo kwa papo ilishuhudiwa huduma ya One Network ikianza Saudi Arabia, nchi yenye miji miwili mitakatifu ya Mecca na Madina.
“Kupanua wigo wa huduma ya One Network kwa Saudi Arabia ni hatua muhimu kwa Zain na hii inadhihirisha tunatekeleza matarajio yetu ya kuwa moja ya kampuni kubwa 10 za mawasiliano ya simu zinazoongoza duniani, na hata kampuni kutoka mabara mengine hazitatuzuia kufanya hivyo," alisema Magavilla.
"Kutokana na kupanua wigo wa huduma zetu Saudi Arabia, Zain tunadhihirisha tunavyowajibika kwa wateja wetu kwa kutoa huduma bora za simu na kuwarahisishia watu mawasiliano na biashara na shughuli mbalimbali, kitu ambacho ni muhimu kwa Zain katika kutekeleza kauli mbiu ya wonderful world (Ulimwengu Maridhawa),"
aliongeza.
Huduma ya One Network ya Zain ndiyo kitu ambacho kinapaswa kuangaliwa kwa hali ya juu kabisa katika mageuzi ya mfumo mpya wa kampuni. Huduma ya One Network hivi sasa inapatikana katika nchi 16 barani Afrika na Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na; Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria, Niger, Chad, Malawi, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Congo Brazzaville, Burkina Faso na Sudan.
Mashariki ya Kati, huduma ya One Network inapatikana katika nchi za Jordan, Bahrain, Iraq na Saudi Arabia.Wateja wote wa Zain barani Afrika na Mashariki ya Kati aliounganishwa katika huduma ya prepaid na postpaid, wanatumia One Network na hivi sasa wanaweza kusafiri kwenda Saudia Arabia wakitumia simu zao, taifa ambalo linaunganisha Afrika na Mashariki ya Kati, bila kutozwa bei zaidi ya ile ya kawaida na bila kulipia gharama ili kupokea simu zinazoingia.
Wateja wa Zain pia wanaweza kuingiza pesa kwenye simu zao wakiwa Saudi Arabia bila kununua kadi kutoka nchi anayotoka na zaidi ya vituo 150,000 barani Afrika na Mashariki ya Kati vinatoa huduma kwa wateja wa Zain popote walipo.
“Wateja wanaweza kupiga na kupokea simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa gharama za kawaida, kupokea bure simu zinazopigwa kutoka katika moja ya nchi 16 zilizounganishwa na huduma ya One Network.
Huduma ya One Network kwa wateja wa prepaid inatolewa moja kwa moja katika nchi zote, na haihitaji mteja ajisajili wala kulipia ada," alisema Magavilla.Zain inatambulika kwa kuongoza katika mageuzi ya teknolojia ya huduma ya mawasiliano ya kisasa kwa wateja inaowatumikia. Zain ilikuwa ya kwanza kuzindua huduma ya ‘One Network’ kwa zaidi ya watu milioni 100 nchini Kenya, Tanzania na Uganda mwaka 2006, na inaahidi kuendelea kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wateja wa Zain.
"Zain itaendelea kuwa mwasisi wa huduma ya ‘One Network’, ambao ni mtandao wa kwanza duniani usio na mipaka, huduma ambayo kwa mara ya kwanza inapatikana katika mabara mawili tofauti – Afrika na Mashariki ya Kati," alisema Magavilla.Lengo bora zaidi la Zain ni kuhakikisha inawasaidia watu wake kupata mawasiliano bora, kushirikiano kwa pamoja, kupanua wigo wa biashara na kufurahia mafanikio.


Toa Maoni Yako:
0 comments: