JK afurahishwa Mwenge wa Olimpiki kukimbizwa nchini

Rais Jakaya Kikwete jana (Ijumaa, Aprili 4, 2008) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China katika Tanzania, Bwana Liu Xinsheng. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu mjini Dar es Salaam.Katika mazungumzo hayo, Mhe Rais na Balozi Xinsheng wamezungumzia uhusiano wa muda mrefu na wa kindugu kati ya nchi hizo mbili.Balozi Xinsheng pia ametumia mazungumzo hayo kumwelezea Mhe Rais kuhusu Mwenge wa Olimpiki ambao utakimbizwa nchini Aprili 13 mwaka huu.Tanzania ni moja ya nchi 20 duniani, na nchi pekee katika Bara la Afrika, ambako mwenge huo utakimbizwa katika mzunguko wake wa dunia kabla ya kurejea Beijing, China tayari kwa Michezo ya Olimpiki inayofanyika nchini humo baadaye mwaka huu.Mhe Rais amefurahishwa na uamuzi wa China kuiteua Tanzania kuwa moja ya nchi ambako Mwenge huo utakimbizwa na kusema kuwa hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania.Wakati huo huo, Mhe Rais pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji wa Hamburg, Ujerumani, Bwana Jurgein Gothardt.Katika mazungumzo hayo, Bw. Gothardt amemweleza Mhe Rais kuhusu jitihada ambazo anazifanya katika kupata nyenzo za kuweza kutengeneza na kutunza baadhi ya majumba ya kale na ya kihistoria katika mji wa Bagamoyo.Mhe Rais amemshukuru Gothardt kwa jitihada zake na kumhakikishia kuwa Tanzania itafanya kila linalowezekana katika kusaidia juhudi hizo za kulinda na kudumisha historia ya nchi hii.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: