Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Serikali imeitaka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kuendelea kutoa elimu kuhusu ulinzi wa faragha na taarifa binafsi kwa wananchi katika maeneo yote ya nchi, ikiwemo mijini na vijijini, ili kuhakikisha kila Mtanzania anaelewa haki zake katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Fatuma Kilovya, wakati akifunga Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi lililofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam na kukutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali.
Bi. Kilovya amesema suala la ulinzi wa faragha na taarifa binafsi linapaswa kuwa ajenda ya kitaifa kutokana na nafasi yake katika kujenga uchumi wa kidijitali na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo, "Faragha Yako, Ni Jukumu Letu," inapaswa kuwafikia wananchi wote, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi na kuheshimu haki za faragha.
"Faragha si chaguo bali ni haki ya msingi katika jamii ya kidijitali. Ulinzi wa taarifa binafsi ndiyo msingi wa kujenga imani kati ya wananchi, Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara katika mazingira ya kidijitali," alisema Bi. Kilovya.
Aidha, ameipongeza PDPC kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa, hususan kutoka Kenya na Uganda, akisema ushirikiano huo unasaidia kujenga mazingira salama ya matumizi ya data na kuimarisha ulinzi wa faragha barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkalia, amesema Tume imepanga kufanya kongamano hilo kila mwaka ili kujadili maendeleo ya teknolojia na changamoto mpya zinazoibuka katika eneo la ulinzi wa taarifa binafsi.
Dkt. Mkalia amesema lengo la mikutano hiyo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili mwenendo wa teknolojia na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha taarifa binafsi za wananchi zinalindwa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Ameongeza kuwa Julai 13 mwaka huu, PDPC kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania itazindua kozi maalumu ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi watakaothibitishwa kitaaluma ili kuongeza wataalamu wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za ulinzi wa taarifa binafsi.
"Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani kuwa taarifa zao zinalindwa ipasavyo na taasisi zinazozihifadhi zina wajibu wa kuhakikisha usalama wake," alisema Dkt. Mkalia.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Balozi Adadi Rajabu, amewataka washiriki wa kongamano hilo kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi na kuhakikisha elimu waliyoipata inawanufaisha wananchi katika maeneo yao.
Balozi Adadi amesema washiriki walikubaliana kuwa kuna haja ya kuendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni za ulinzi wa taarifa binafsi, kuongeza elimu kwa wananchi, kuhimiza uwajibikaji kwa taasisi na kampuni zinazoshughulikia taarifa za watu pamoja na kuhakikisha Serikali inaendelea kulinda taarifa za wananchi bila kuathiri maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kidijitali.
Kongamano hilo liliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, kampuni za mawasiliano, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wahadhiri, wanafunzi, wataalamu wa teknolojia, sekta ya afya, sheria pamoja na asasi za kiraia, kwa lengo la kujadili mustakabali wa ulinzi wa faragha na taarifa binafsi nchini.





































Toa Maoni Yako:
0 comments: