Aidha limewataka ndugu wote wenye ualbino nchini Tanzania na duniani kote, wasikate tamaa na kuwakumbusha waendelee kuamini katika uwezo wao,kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na kutimiza ndoto zao na kwamba Dunia inahitaji mchango, vipaji na uwezo wenu.
Hayo yamesemwa na Boniventura Mwalongo ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO)
na Mjumbe wa Kamati Maalumu ya Pamoja ya Kushughulikia Changamoto za Watu Wenye Ualbino nchini alipokuwa akitoa salamu katika Maadhimisho ya kimataifa ya kuongeza uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika Juni 13,2026.
“TRAMEPRO inapenda kuwahakikishia watu wote wenye ualbino kwamba itaendelea kuwa sauti yao na mshirika wao katika kutetea haki, usawa, heshima na maendeleo yao. Ahadi yetu ni kwamba kamwe hatutawasaliti katika kusimamia haki zenu na haki za binadamu kwa ujumla.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali, Bunge, taasisi mbalimbali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa watu wenye ualbino wanapata ulinzi, heshima, fursa na haki zote wanazostahili kama raia wengine,”amesema na kuongeza "Utu, usawa, upendo na uhifadhi wa mazingira ni msingi wa maendeleo endelevu na jamii yenye amani kwa wote."
Akieleza zaidi kuhusu maadhimisho hayo amesema TRAMEPRO inaamini siku hiyo ni fursa muhimu ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu haki, usawa, usalama, afya na ustawi wa watu wenye ualbino, pamoja na kupinga ubaguzi, unyanyapaa na vitendo vyote vya ukatili vinavyokiuka haki zao za msingi.
Pia maadhimisho hayo yanakumbusha wajibu wa pamoja wa kujenga jamii inayoheshimu utu, usawa na haki za kila mwanadamu bila kujali tofauti zake za kimaumbile.
“TRAMEPRO inatoa pongezi kwa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Albinism Sports Club, Serikali, Bunge, wataalamu wa tiba asili, wadau wa afya, elimu, michezo na mazingira pamoja na wanachama wote wa TRAMEPRO kwa mchango wao katika kuimarisha ustawi, usalama na maendeleo ya watu wenye ualbino nchini.”
Wakati huo huo Mwalongo ametumia maadhimisho hayo kueleza wanatambua na kupongeza mechi ya kirafiki iliyochezwa Juni 6,2026 kati ya Bunge Sports Club na Albinism Sports Club, ambayo imeendelea kuwa mfano bora wa matumizi ya michezo katika kuhamasisha ushirikishwaji, mshikamano, uelewa na mapambano dhidi ya ubaguzi kwa watu wenye ualbino.
Tukio hilo limeonesha michezo ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.Tunatoa shukrani za dhati kwa viongozi wa Bunge Sports Club, Waheshimiwa Wabunge na wadau wote walioshiriki kufanikisha tukio hilo muhimu.
Aidha, wanaguswa na moyo wa upendo, utu na kujali uliooneshwa na Salma Kikwete, ambaye baada ya kuguswa na hali halisi ya baadhi ya wachezaji wa Albinism Sports Club alionesha moyo wa kuwafariji na kuwasaidia. Kitendo hicho ni mfano wa kuigwa katika kujenga jamii yenye huruma, mshikamano na usawa.
“Pia tunatoa shukrani kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)kwa kuwezesha upatikanaji wa miche iliyotumika katika zoezi hilo. Mchango huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, mashirika ya kiraia na wananchi katika kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.”



Toa Maoni Yako:
0 comments: