
Na Mwandishi Wetu.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva, ameongoza zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Lindi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kujiandaa na maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani pamoja na Wiki ya Upandaji Miti Kitaifa.
Zoezi hilo lilifanyika Machi 4, 2026 kwa ushirikiano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Lindi, viongozi wa Serikali ya Kata ya Mtanda, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtanda, pamoja na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lindi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Wilaya ya Lindi, Gasper Vincent, alisema kuwa taasisi hiyo imezalisha zaidi ya miche 200,000 kwa msimu wa upandaji miti wa mwaka 2026 ili kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira katika Manispaa ya Lindi. Alibainisha kuwa kati ya miche hiyo, miche 1,000 imewasilishwa katika Shule ya Sekondari Lindi kwa ajili ya zoezi hilo la upandaji miti.
Aidha, zoezi hilo liliongozwa kwa karibu na Diwani wa Kata ya Mtanda, Mhe. Iddi Lulida, ambaye alishirikiana na viongozi wa kata pamoja na wanafunzi kuhakikisha miti inapandwa na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.
Maadhimisho ya Wiki ya Upandaji Miti Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Manispaa ya Lindi kuanzia Machi 12 hadi 21, 2026, ambapo wananchi wa Wilaya ya Lindi wamehimizwa kuendelea kupanda miti, kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.







Toa Maoni Yako:
0 comments: