~ Wananchi watangaza kumtetea Rais Samia kwa gharama yoyote

Na Mwandishi Wetu 

Wananchi wa Kata ya Msikisi wameonyesha mshikamano wa kipekee kwa kuzindua ofisi ya kwanza na ya kihistoria ya TK Movement, wakiahidi kumlinda na kumtetea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa gharama yoyote ile.

Uzinduzi huo, uliofanyika katika Kijiji cha Miwale, uliandaliwa kwa nguvu za wananchi wenyewe na kufanywa rasmi na Afisa Tarafa wa Lisekese, Emmanuel Shilatu, ambaye aliwasihi Watanzania kuongeza moyo wa utaifa na uzalendo.

“Nawapongeza kwa kuhakikisha tunapata ofisi ya kwanza ya TK Movement. Ndugu zangu, akikuuliza mtu Tanzania tunacho nini, mwambie tuna amani, tuna maendeleo, na tuna Rais Samia—Mzalendo, mchapa kazi, hodari, mtekelezaji na mfuatiliaji. Mwonyesheni miradi ya afya, elimu, maji, miundombinu, na pembejeo za kilimo mnazopewa bure na Rais Samia. Hakikisheni mnawaeleza watu utekelezaji wa Ilani ya CCM unaofanywa na Serikali,” alisema Shilatu.

Aidha, aliwataka wananchi kudumisha amani na kuepuka vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

Kwa upande wake, kijana Rauphu Said alisema wao kama vijana wameamua kuilinda serikali iliyopo madarakani na kumtetea Rais Samia kutokana na maendeleo makubwa yanayoonekana kote nchini.

“Tunayaona maendeleo haya, na kwa wivu wa maendeleo haya, tumeamua kusimama bega kwa bega kumlinda na kumtetea Rais wetu,” alisema Rauphu.

TK Movement ni mtandao unaohamasisha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ili kuchochea kasi ya ustawi wa Taifa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: