Na Emmanuel Mbatilo, Michuzi TV – Dodoma
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imemuidhinisha Bi. Zahra Muhidin Michuzi kuwania nafasi ya Ubunge wa Viti Maalumu Wanawake kupitia Mkoa wa Tabora, katika uteuzi wa awali wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Zahra ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji (DED) aliyehudumu katika halmashauri tatu tofauti nchini — Meatu (Simiyu), Ifakara (Morogoro), na Geita (Geita Mjini) — ni miongoni mwa wagombea tisa waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, akiwania sambamba na akina mama wenye rekodi mbalimbali za kiuongozi wakiwemo Aziza Sleyum Ally, Jaqueline Kainja Andrew, Christina Solomon Mndeme, Zuena Mohamed Yusuph, Dkt. Bayoum Awadhi Kigwangala, Mkuwe Abdul Issale, na Rebeka Joseph Kashindy.
Zahra anatambulika kwa mtindo wake wa uongozi wa karibu, usimamizi makini wa miradi ya maendeleo, na uwezo mkubwa wa kujenga mshikamano kati ya viongozi na wananchi. Kabla ya kuwa DED, alitumikia nafasi ya Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma ambako alijijengea heshima kubwa kwa kuimarisha mifumo ya kiutawala na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa hatua yake ya sasa ya kuingia katika ulingo wa kisiasa kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Zahra analeta uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika sekta ya umma, huku akilenga kuibua na kusukuma mbele ajenda za maendeleo zinazowahusu wanawake, vijana, na jamii kwa ujumla.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaiona hatua hii kama mwanzo wa sura mpya ya ushiriki wa wanawake waliokomaa kitaaluma katika siasa za uwakilishi na uundaji wa sera nchini. Wanabainisha kuwa uzoefu wa Zahra katika utumishi wa umma unaweza kuwa nguzo muhimu katika kuleta mjadala wenye tija bungeni.
Kama atateuliwa na hatimaye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, matarajio ni kwamba atakuwa sauti madhubuti ya wanawake wa Mkoa wa Tabora na mfano wa kuigwa kwa watendaji wa umma wenye ndoto ya kutoa mchango katika uongozi wa kisiasa.



Toa Maoni Yako:
0 comments: