Na Emmanuel J. Shilatu
Tanzania ya sasa ni tofauti kabisa na ile ya wakati ule tunapata Uhuru mnamo Disemba 9, 1961. Imebadilika sana kwenye nyanja zote za kimaisha na hata katika awamu zote za Urais zilizoongoza nchi. Si awamu ya Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete na hata hii ya Magufuli kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye kila awamu.
Si demokrasia, si uhuru wa habari, si masuala ya miundombinu, si masuala ya wasomi yaani kila idara imekuwa na mabadiliko sana. Tunaweza kuitofautisha Tanzania ya leo mwaka 2017 na ile ya wakati tunapata uhuru mwaka 1961 kwa kutumia vigezo vya kitakwimu.
Twende sawa. Mtandao wa barabara mwaka 1961 ulikuwa ni Kilomita 33,600 ambapo kilomita 1360 ndizo zilikuwa za lami. Leo hii kuna kilomita 122,500 kati ya hizo kilomita 12,679.55 zina lami. Hata upande wa Madaraja leo hii tuna madaraja 8070 kati ya hayo 77 ni madaraja makubwa.
Vituo vilivyokuwa vikitoa huduma ya afya mwaka 1961 vilikuwa 1095, leo hii kuna jumla ya vituo zaidi ya 7293 vikubwa na vidogo vinavyotoa huduma ya afya kote nchini.
Idadi ya shule nazo pia zimeongezeka. Shule ya Msingi mwaka 1961 zilikuwa 3100, leo hii kuna zaidi ya shule za msingi 17379. Upande wa shule za sekondari mwaka 1961 zilikuwa 41, leo hii kuna zaidi ya shule za sekondari 4817.
Mwaka 1961 kuna na Chuo kikuu kimoja tu, leo hii Tanzania kuna zaidi ya vyuo vikuu 48.
Hata kwa upande wa kuzalisha idadi ya Wasomi napo pia kuna maendeleo makubwa yametokea. Mathalani upande wa Madaktari Wazalendo waliosajiliwa mwaka 1961 walikuwa 12, leo hii nchini kuna Madktari waliosajiliwa 9343.
Upande wa Wahandisi Wazalendo mwaka 1961 walikuwa 2, leo hii wapo zaidi ya Wahandisi 19164 waliosajiliwa. Hata upande wa Makandarasi Mwaka 1961 kulikuwa na Makandarasi Wazalendo 2, leo hii mwaka 2017 kuna Makandarasi Wazalendo zaidi ya 9350 waliosajiliwa.
Tunaposema Tanzania ya leo ni tofauti na ile ya mwaka 1961 inabidi Watanzania tutembee vifua mbele maana kuna maendeleo chanyA+ kila mahali si maji umeme, utalii, kilimo, mifugo, uvuvi, madini n.k
Mpaka sasa bado najiuliza wale wanaosema hakuna cha maana kilichofanyika tangu tupate uhuru, hawana macho ya kuona, ama hawana masikio ya kusikia maendeleo haya, au Bongo zao zimeamua kuwa wapotoshaji wa maksudi?
Najivunia maendeleo chanya tuliyonayo nchini ambayo yameibadilisha sana Tanzania ambayo pia yamekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania. Leo hii umri wa kuishi Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 37 ya mwaka 1961 mpaka miaka 61 kwa mwaka huu 2017.
Najivunia Serikali zote zilizoongoza nchini ambazo kila mmoja amechangia ongezeko la maendelo chanya nchini.
Uzalendo ni pamoja na kujivunia maendeleo tuliyonayo.
Matokeo chanyA+
*Shilatu E.J*
0767488622
Toa Maoni Yako:
0 comments: