Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Waendesha pikipiki za kusafirisha abiria (bodaboda) wilayani Nachingwea wameaswa wasikubali kutumiwa na wanasiasa nakufanywa ngazi ya kufikia malengo yao yakisiasa.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na mkurugenzi mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya kupambana na umasikini na utunzaji mazingira (APEC), Respicius Timanywa.Wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya usalama barabarani iliyofanyika katika kijiji cha Chiola wilaya ya Nachingwea.

Timanywa alisema madereva bodaboda ni kundi lenye nguvu katika jamii kutokana na kuundwa na vijana. Hivyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa natabia ya kuwalaghai ili wawaunge mkono kwa kuwataka washiriki kutekeleza vitendo vya uvunjifu wa sheria. Ikiwamo kushiriki maandamano na mikutano isiyo halali.

Mkurugenzi huyo ambae taasisi yake inashugulika pia na kupunguza maafa kwa waendesha pikipiki, alisema vijana hawana budi kukataa kutumika kufanya vitendo vitakavyo vuruga amani na utulivu uliopo nchini kwa maslahi ya wanasiasa.

Badala yake wajiwekee malengo ya kufikia maendeleo kwakufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

"Anzisheni vikundi vya ujasiriamali na fungueni akaunti ili muweze kuungwa mkono na serikali, muweze kukopeshwa kupitia fedha za mifuko ya vijana na wanawake," alisisitiza Timanywa.

Aidha alitoa wito kwa serikali iwatambue waendesha bodaboda kuwa nimiongoni mwa watu wanaoweza kuchangia uchumi wa taifa kupitia kazi wanayofanya, iwapo wataandaliwa mazingira mazuri ya kufanya kazi yao.

Alibainisha mchango wa vijana hao utatokana na kodi kupitia kazi wanayofanya. Hata hivyo kwa mazingira ya sasa wanajiona kama wametengwa.

"Sasa hivi hawana sehemu ya maalumu ya kuegesha pikipiki zao na hawana vituo, wanapigwa na jua na mvua ikinyesha wanahangaika, serikali iwajengee vituo wanaweza kuwa walipaji wazuri wa kodi," alisema Timanywa.

Alisema kunahaja ya vijana wanaohitimu mafunzo kupewa leseni haraka ili waanze kulipa kodi na kuchangia pato la taifa. Hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ipo katika harakati kubwa za kuleta maendeleo ya nchi kupitia ukusanyaji makini wa mapato na kuziba mianya wizi na ufisadi.

Mbali na hayo, mkurugenzi huyo alitoa wito kwa serikali pitia jeshi la polisi kuendelea kutoa ushirikiano na taasisi ili kuendelea kuwapa elimu waendesha bodaboda. Kwani wasipopata elimu wataendelea kuwa chanzo cha ajali nakusababisha madhara kwa taifa kutokana na kupoteza nguvu kazi.

Akiongeza kusema hata waendesha bodaboda watakuwa hawanufaiki na kazi hiyo. Kwasababu sehemu kubwa ya mapato yao yatatumika kulipa faini kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Nae ofisa tawala wa wilaya ya Nachingwea, Stephen Mbije, ambae alimuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo, aliwaasa vijana hao kujiunga na mfuko wa jamii wa bima ya afya ili waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu. Huku akiwaomba waanzishe vikundi vya ulinzi shiriki vya jamaii, ili kukabilina uhalifu katika maeneo yao.

Kwa upande wake, katibu wa washiriki hao, Deograsia Litimba, alisema licha ya mafunzo hayo kuwafanya wazielewe sheria za usalama barabarani lakini pia yamesababisha wabaini kuwa sababu ya mahusiano hafifu baina yao na jeshi la polisi ni wao kutozitambua sheria.

Huku akibainisha kuwa mafunzo hayo ambayo yalitolewa na APEC kwa kushirikiana na jeshi hilo yamesababisha wawe na mahusiano mema nakuwa wanafamilia.

Mafunzo hayo ya wiki moja yalikuwa na washiriki 220 waliotoka katika za Mkoka, Kipara Mtua, Kipara Mnero, Chiola, Marambo, Ruponda na Mnero Ngongo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: