Yapo mambo ambayo huwaumiza watu vichwa yamkini yakiwa ni mambo madogo na ya kawaida. Tatizo mara nyingi huwa ni taarifa. Taarifa zikimfikia mtu ndipo huhisi jambo ambalo alikuwa halijui kuwa ni jepesi. Lakini kabla ya taarifa mtu huendelea kufikiria jambo hilo kwa ugumu.
Katika kipindi kama hiki kuwa na kitu kama pasipoti si jambo la anasa au ufahari tena isipokuwa ni jambo ambalo limeishaingia katika matumizi ya kawaida ya kila siku ya walio wengi. Hii ni kutokana na kukua kwa biashara za kimataifa, mawasiliano, utalii, usafirishaji na kila kitu ambacho husababisha watu kutoka nchi moja hadi nyingine. Kwasasa kuwa na pasipoti hata kama huna safari ya hivi karibuni ni jambo muhimu sana.
Yamkini usisubiri ikutokee safari ya ghafla halafu ndio uanze kukimbizana na pasipoti. Pasipoti inayo manufaa mengi lakini moja ni kuwa pasipoti ni mali kama mali nyingine. Pasipoti inaweza kumdhamini mtu kama mali nyingine inavyoweza kumdhamini mtu. Pasipoti ni amana tena amana ya kuaminika. Ni kutokana na umuhimu huu nikaona leo nieleze pasipoti na namna ya kupata pasipoti.
1. PASIPOTI HUOMBWA NA MWOMBAJI LAKINI HUBAKI MALI YA SERIKALI.
Hakuna mtu mwenye umiliki wa kudumu wa pasipoti. Kwa mujibu wa sheria licha ya kuwa pasipoti hutolewa kwa jina na maelezo ya mwombaji,hati hiyo hubaki kuwa ni mali ya serikali. Hii ndio sababu serikali huweza kumnyanganya mtu pasipoti panapo jambo fulani. Ni kwakuwa pasipoti ni mali yake. Wewe mwombaji uliyepewa pasipoti unayo haki ya matumizi na uhifadhi wake lakini mmiliki mkuu ni serikali.
2. ILI KUPATA PASIPOTI UNAHITAJI KUWA NA VITU HIVI.
( a ) Cheti cha kuzaliwa, hati ya kiapo au cheti cha uraia wa kuandikishwa cha mwombaji.Cheti cha kuzaliwa ni hivi vyeti vya kawaida ambavyo hutolewa mahospitalini au mamlaka nyingine baada ya kuzaliwa kwa mtu. Katika kipindi hiki wapo wengine wamekwisapata vyeti vya uraia. Cheti cha uraia chaweza kutumika kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa. Pia tumesema hati ya kiapo. Hii hutolewa kwenye ofisi za wanasheria. Mwombaji huwa anaapa pamoja na mambo mengine kuthibitisha kuwa taarifa anazozitoa ni za kweli kwa dhati yake. Pia tukasema vyeti vya uraia wa kuandikishwa. Hivi wanavyo raia wa Tanzania ambao si wa kuzaliwa. Katika kuomba kupata pasipoti nao hutakiwa kuwa navyo.
( b ) Cheti cha kuzaliwa, hati ya kiapo au cheti cha uraia wa kuandikishwa cha
mzazi au wazazi wa mwombaji. Hapo juu tumeona vitu kama hivihivi lakini ilikuwa ni kwa mwombaji wa pasipoti mwenyewe. Hivi hapa sasa ni kwa ajili ya mzazi wa mwombaji. Vile vitu vyote alivyowasilisha mwombaji pale juu ndio vilevile anavyopaswa kuwasilisha mzazi wa mwombaji. Si kwamba mzazi mwenyewe ndio anapeleka vitu hivyo hapana, wewe mwombaji ndio unabeba vitu hivi kwa niaba ya mzazi. Hapa mzazi ni yeyote anaweza kuwa baba au mama.Lengo lake ni kutaka kujua historia fupi ya nasaba ya mzazi wa mwombaji.
( c ) Inahitajika picha ya hivi karibuni ya pasipoti size. Sharti kubwa waliloweka hapa ni kuwa picha hiyo isiwe katika fremu. Fremu hapa si tu ile fremu ya kawaida tuliyoizoea bali pia hata pasipoti kuwa na maringo au mapambo ya kuzungushia pembeni nayo ni fremu kwa maana hii. Pasipoti iwe mnyooko(plain) isiwe na mbwembwe zozote.
( d ) Iwapo mwombaji ana umri wa chini ya miaka kumi na nane (18), wazazi walezi wawasilishe ridhaa ya maandishi. Nyaraka hii ya ridhaa ya maandishi huandaliwa na mwanasheria.Hii ni kusema kuwa utaratibu wa mtu mzima aliyevuka miaka kumi na nane ni tofauti na mtu aliye chini ya miaka hiyo katika kupata pasipoti. Baada ya kukamilisha vitu hivi kama nilivyoeleza basi hatua inayofuata ni kufuata utaratibu huu chini.
3. FOMU ZA MAOMBI HUPATIKANA WAPI.
Ofisi za uhamiaji ndipo zilipo fomu za maombi ya pasipoti. Hii ni popote Dar es salaam au mikoani. Suala la msingi ni kuwa ofisi hiyo iwe ya uhamiaji utapata fomu hizo. Utachukua fomu hiyo utaijaza na baada ya kuijaza itawasilishwa kwa mkurugenzi wa uhamiaji. Aidha suala jingine la msingi ni kuwa fomu hii itawasilishwa sambamba na nyaraka zote zinazotakiwa kama ilivyoelezwa hapo juu.
4. BEI YA PASIPOTI NI KIASI GANI.
Ada rasmi ya kupata pasipoti ni fedha za Kitanzania kiasi cha shilingi 50,000/= ( Elfu hamsini tu). Aidha kwakuwa wanasheria ndio hushughulika na kutafuta pasipoti basi bei yao haiingizwi katika ada rasmi ya serikali kama nilivyoieleza hapo juu.
5. UNAWEZA KUOMBWA VIAMBATANISHO VYA ZIADA.
Jambo jingine ni kuwa safari zimeainishwa kwa namna mbalimbali.Ukisoma nyuma ya fomu ya maombi utaliona hili. Kutokana na hilo wakati mwingine waweza kuombwa viambatanisho vya ziada. Hii ni kutokana na utofauti wa safari. Hii ni kusema kuwa yawezekana mwombaji akaombwa viambatanisho viitwavyo viambatanisho “maalum”. Hivyo basi mtu asishangae kukutana na kitu cha namna hiyo.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIAANAPATIKANA KWA NAMBA 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
Toa Maoni Yako:
0 comments: