RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuwatumia wataalamu wazalendo katika kazi za kitaalamu za Serikali huku akiupongeza uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kufanikisha mambo mbali mbali yenye mnasaba na utekelezaji malengo na majuku yaliyowekwa na Ofisi hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mkutano kati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, huko Ikulu mjini Zanzibar, mkutano wenye lengo la kuangalia Utekelezaji wa Malengo ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo hiyo kwa robo mbili kati ya Julai hadi Disemba 2014.

Katika maelezo yake Dk. Shein, alipongeza hatua zilizochukuliwa na Ofisi hiyo katika kuhakikisha malengo yaliwekwa yanafikiwa pamoja na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ambapo pia, alieleza umuhimu wa kuwatumia wataalamu wazalendo ambao wamesomeshwa na Serikali hii badala ya kujikita zaidi na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kuusisitiza uongozi wa Wizara hiyo akiwemo Waziri na Katibu Mkuu wake kuendelea na utaratibu uliwekwa na Serikali wa kutoa taarifa kwa wananchi kwa muda uliopangwa kupitia vyombo vya habari ili kuwaeleza mafanikio yaliopatika.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na kupata mafanikio makubwa ambayo inapaswa wananchi kupewa taarifa juu ya mambo hayo sambamba na kuelezwa changamoto zilizopo na jinsi juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha na kuendeleza huduma za kijamii na miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya maji ambayo licha ya changamoto zilizopo lakini huduma hiyo imeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Mapema akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Malengo ya Mpango Kazi wa Bajeti ya Ofisi hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame alieleza majukumu, malengo, mafanikio na changamoto zilizopo na juhudi zinzochukuliwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ndani ya Idara za Ofisi hiyo.

Katika kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali za umma yanafanyika kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji Dk. Mwinyihaji alisema kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar imekamilisha Ukaguzi wa Hesabu katika Wizara na Mashirika ya Serikali.

Dk. Mwinyi alisema kuwa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2012/2013 imeonesha kuwa kuna mabadiliko makubwa katika matumizi ya fedha na rasilimali za umma.

Alisema kuwa taasisi nyingi na Idara za Serikali hivi sasa zinazingatia na kufuata taratibu za matumizi za fedha na manunuzi na uuzwaji wa mali za serikali, kuweka kumbukumbu na kufunga hesabu za mwaka kwa wakati.

“Hapa tunatoa pongezi kwako mwenyewe Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa jinsi unavyotenga muda wako kujadili ripoti za CAG na jinsi unavyowaelekeza Watendani Wakuu wanavyopaswa kusimamia Wizara na Taasisi zao’,alisema Dk. Mwinyihaji.

Aidha, Dk. Mwinyihaji alisema kuwa Serikali imepitisha Sera ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi (PPP) ambapo miongoni mwa vipaumbele katika Sera hiyo ni kuimarisha huduma na ujenzi wa miundombinu ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.

Pamoja na hayo, Waziri Mwinyihaji alieleza kuwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaendelea na ukusanyaji wa taarifa za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2014/2015.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyihaji alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa niaba ya uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuimarisha ustawi wa jamii zikiwemo huduma za afya, elimu na nyenginezo hasa tamko lake la hivi karibu na kuondoa michango maskulini sambamba na tamko la kutotozwa fedha akina mama wanaofika hospitali kwa ajili ya kujifungua.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mazee alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo kwa juhudi iliyozichukua katika uwasilishaji mzuri wa MpangoKazi wake sambamba na utekelezaji wa malengo na majukumu kwa Ofisi hiyo. Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: