Balozi wa Umoja Ulaya nchini, Filiberto Sebregondi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Richard Sezibera wakibadilishana hati za makubaliano ya msaada wa fedha zinazotolewa na umoja huo kwa ajili ya kuiwezesha EAC kufanya uangalizi wa uchaguzi katika nchi za Burundi na Tanzania utakaofanyika mwaka huu, hafla hiyo imefanyika leo jijini Arusha.
Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Jumuiya ya Ulaya (EU), imetoa Euro 5 milioni sawa na Sh 9.7 bilioni kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kusaidia shughuli za uratibu, ufuatiliaji na uangalizi wa zoezi la uchaguzi mkuu katika nchi za Tanzania na Burundi.
Mkataba wa makubaliano ya kutoa kiasi hicho cha fedha umesainiwa leo jijini Arusha kati ya Kiongozi wa EU nchini, Balozi Filiberto Sebregondi na Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera.
Wakizungumza muda mfupi baada ya kutiliana saini msaada huo ambao ni kati ya msaada wa zaidi ya Euro 85 milioni itakayotolewa na EU kwa EAC kwa ajili shughuli za uchaguzi na ujenzi wa demokrasia kufikia 2020, viongozi hao wawili wamesema Jumuiya za Kikanda za EU na EAC zinashabihiana katika mambo mengi ya msingi kuhusu haki za kijamii.
Amesema kwa EU, suala la uangalizi katika mchakato wa uchaguzi ni suala muhimu kwa sababu siyo tu huwezesha urekebishaji wa makosa yanayojitokeza, bali pia hujenga demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria wakati wote wa uchaguzi.
Kwa upande wake, Dk Sezibera licha ya kushukuru, pia amesema msaada huo utazidi kuimarisha proramu ya ufuatiliaji, usimamizi na uratibu wa masuala ya chaguzi za kidemokrasia miongoni mwa nchi wanachama.
“EAC tumejiwekea mipango na mikakati ya kufuatilia, kuratibu na kuangalia chaguzi zote zinazofanyika ndani ya nchi zote tano wanachama kuanzia mwaka 2013 hadi 2018,” alisema Dk Sezibera
Amesema mpango huo ulianzia katika uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka juzi, ukafuatiwa na uchaguzi wa wabunge nchini Rwanda mwaka jana na mwaka huu uchaguzi mkuu katika nchi za Tanzania na Burundi kabla ya kukamilishia Uganda mwakani.
Pia zitalipia gharama za waangalizi kutoka EAC, watumishi wakataopelekzwa Burundi na Tanzania wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Nchi wanachama wa EAC, Tanzania, Kenya Uganda, Rwanda na Burundi, zimeunda programu maalum ya masuala ya uchaguzi unaoratibiwa na Sekretarieti ya EAC kuhakikisha chaguzi zote ndani ya Ukanda huo zinakuwa huru, haki na za kidemokrasia.
Toa Maoni Yako:
0 comments: