Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akionyesha picha za viongozi wa Panya Road kwa wanahabari.
Baadhi ya Panya Road waliokamatwa.

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu 510 wakiwemo viongozi watatu wa kundi linalojihusisha na uhalifu la ‘Panya Road’ .

Watu hao wamekamatwa katika operesheni inayoendeshwa na jeshi hilo, kupambana na uhalifu.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema jana kuwa watuhumiwa hao, ni pamoja na watuhumiwa 36 waliokamatwa juzi, kufuatia vurugu iliyotokea Ijumaa iliyopita.

Alisema chimbuko la Operesheni hiyo, inayoendeshwa na wakuu wa Polisi wa Mikoa ya Kipolisi ya Temeke, Kinondoni na Ilala, wapelelezi na askari wa kiintelijensia ni matukio yaliyowahusisha vijana hao na kusababisha tafrani kwa wananchi mbalimbali wa jiji la Dar es Salaam.

Alitaja viongozi wa kundi hilo wanaoshikiliwa kuwa ni Khalfani Said (24) na Said Mohammed (22), wakazi wa Tandale Sokoni katika Manispaa ya Kinondoni na Mohammed Nangula (19), mkazi wa Mburahati kwa Jongo, pia Kinondoni.

Alisema kwamba kazi yao kubwa ni kuwaunganisha na kuratibu uporaji katika maeneo mbalimbali.
Alisema mbali na ‘Panya Road’, operesheni hiyo ambayo itakuwa ya kudumu kuanzia sasa, imewakamata wapigadebe, wacheza kamari na watuhumiwa wengine waliokamatwa katika vijiwe na katika msako wa nyumba kwa nyumba.

“Imegundulika kwamba kila inapotokea kijana ameuawa, wakati wa maziko viongozi hawa wanakuwepo na kuwachochea vijana wenzao kufanya vurugu, kama ilivyotokea Januari 2 katika eneo la Magomeni Kagera ambapo vijana walipambana na polisi baada ya maziko ya kijana mwenzao aliyefariki kutokana na matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi Januari Mosi eneo la Mwananyamala.

“Tunashukuru kwa kuwa baadhi ya wananchi waliweza kutupa ushirikiano wa moja kwa moja kuwabaini wahalifu tunaowashikilia, ni ukweli usiopingika kuwa vijana hawa wanaojihusisha na vitendo viovu wanafahamika kwa wananchi hivyo ni jukumu la wazazi, walezi katika mitaa yote ya Dar es Salaam kujihusisha kikamilifu katika kuwabaini vijana hao ili tuweze kukomesha maovu yao ambayo pia ni kero kwa wananchi,” alisema Kamanda Kova.

Aidha, alisema katika operesheni hiyo, pia watuhumiwa hao walikamatwa na vilevi mbalimbali zikiwemo bangi, lita 150 ya pombe kali aina ya gongo na mabunda matatu ya dawa za kulevya aina ya mirungi.

Alisema katika kuhakikisha msako huo unazaa matunda, jeshi hilo limeweka mpango maalumu wa kuwahusisha moja kwa moja watendaji kuanzia ngazi ya Mitaa, Kata na Tarafa ili waweze kushirikiana na polisi kuweza kuwabaini wahalifu au makundi ya uhalifu wa aina hiyo.

Alisema mpango huo utafanikiwa kutokana na semina elekezi iliyotoa mafunzo hayo, iliyofanyika hivi karibuni kwa watendaji hao katika kukabiliana na matukio hayo.

Aliwataka vijana ambao hawana kazi za kufanya, kutafuta njia nyingine za kuendesha maisha yao na siyo kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na kufanya makosa ya jinai, yanayowafanya baadhi kujiingiza katika makundi hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: