Meneja Mkuu wa Tanzania House of Talent, Mwita Mwaikenda akizungumza kuhusiana na maadhimisho ya miaka kumi ya THT, kulia ni mwakilishi wa kampuni ya MOSAIC, Deo Masagati ambao ndio wadhamini wa shuguli hiyo, na kushoto ni mwanamziki Peter Msechu ambaye ndio mwongozaji wa burudani siku ya tamasha.
Mbunifu wa Mavazi, Ally Remtullah akiongea na waandishi kuhusu uzinduzi wa mradi wa ubunifu na ushonaji unaonzishwa na THT. Kulia ni Peter Msechu, na kushoto ni Lameck Ditto.
Lameck Ditto akiongea na waandishi juu ya maadhimisho ya miaka kumi ya THT
Mkuu wa Masoko wa THT, Michael Nkya akiongea na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya miaka kumi ya THT.
*Kufungua kampuni ya ushonaji na ubunifu wa mavazi
Kituo cha kuzalisha na kukuza vipaji, Tanzania House of Talent, kinatarajia kuadhimisha miaka kumi toka kuanzishwa kwake hapo tarehe Januari 31, 2015 Escape 1 jijini Dar es Salaam.
THT ilianzishwa mwishoni mwa mwaka 2005 kwa lengo la kuwasaidia vijana wenye vipaji, lakini wasio na uwezo wa kujiendeleza wenyewe, kwenye sekta ya sanaa hapa nchini, na toka wakati huo kituo kimekuwa na mafanikio makubwa na mchango wa pekee kwenye kukuza sanaa ya muziki nchini.
Akizungumza wakati wa kuzindua maadhimisho hayo ambayo yatakuwa kwa mwaka mzima, Meneja Mkuu wa Kituo hicho, Mwita Mwaikenda alisema ni heshima kubwa kuweza kusherehekea miaka kumi toka imeanzishwa kwani wameweza kufanikisha mambo mengi makubwa.
‘Tulianzisha kituo hiki miaka kumi iliyopita kwa hakika tukiwa hatuna chochote zaidi ya imani yetu kwenye vipaji vya vijana, na tulianza hatuna hata sehemu ya maana, lakini leo miaka kumi baadaye vijana zaidi ya 3000 wamefaidika na kituo hiki kwa namna moja au nyingine na wameweza kumudu maisha yao na familia zao kutokea kuwa watoto wa mitaani’ alisema Mwita.
THT ikiwa imeanzishwa kama kituo cha kusaidia watoto wa mtaani wenye vipaji, imeweza kukua kwa kipindi cha miaka kumi, na sasa sio tu inazalisha na kukuza vipaji bali imekuwa ikitoa huduma zote kuanzia kuratibu matamasha, kuandaa mpangilio wa burudani, kutengeneza matangazo ya radio na televisheni pamoja na makala na vipindi vya televisheni.
‘THT imeweza kuratibu burudani ya matamasha mbalimbali kama FIESTA, Mkutano wa Smart Partnership, Sensa ya mwaka 2013, Sherehe za miaka 50 ya Muungano pamoja na mikutano na matamasha kadha wa kadha’ alisema Meneja Masoko wa THT, Michael Nkya.
THT imeendelea kukua kwa kuweza kuanzisha studio yake ambayo imeweza kurekodi matangazo, nyimbo za wasanii wote wa THT pamoja na wengine wengi kama Mdogomdogo na Number One Remix ya Diamond, Me and You ya Ommy Dimpoz, Prokoto ya Victoria Kimani na nyingine nyingi.
Kwa sasa THT inatengeneza vipindi mbalimbali vya televisheni kama 69 Records, na vingine vingi vinavyorushwa chaneli za nje huku pia ikijivunia kuwa na maktaba ya nyimbo kubwa zaidi nchini.
‘Shukrani zetu za dhati kwa kweli ni kwa serikali, hasa hasa Mheshimiwa Rais Kikwete, ambaye toka mwanzo alikubali wazo na akaamini mziki unahitaji elimu ya peke yake, lakini pia makampuni mbalimbali ambayo wamekuwa wakitupa kazi pamoja na vyombo vyote vya habari kwa kutuunga mkono siku zote’ alisema Bwana Nkya.
Akielezea kuhusu mwelekeo wa kituo baada ya miaka kumi, Mwita alisema anaamini kituo kimefanya kazi yake tayari kwa kuweza kuchagiza sanaa ya muziki nchini, na sasa ni wakati wa kuendelea kusaidia wadau au vituo vingine kama Mkubwa na Wanawe kufika THT ilipofika.
‘Kimsingi mwaka huu ndio mwaka wa mwisho kuendela kupokea wanafunzi wapya wa kuimba, na mpango wetu ni kuendelea kukuza kituo kwa kuanzisha kampuni ya ushonaji na ubunifu wa nguo kwa kutumia kitenge ambao tunaamini utatoa ajira kwa vijana wengi zaidi hapa nchini’ alisisitiza Mwita.
Kampuni ya ubunifu na ushonaji kwa kutumia vitenge, tayari ishaanza mchakato wake kwa kuhusisha wadau wa biashara ya vitenge, na mbunifu mahiri Ally Remtullah, mwanamitindo Flaviana Matata wakiwa ndio walezi na wasimamizi wa mradi ambao utaanza na wabunifu wanaochipukia Neyonce pamoja na Adam Mchovu.
‘Kwa kuanza mradi utapeleka wabunifu nchini China ili wakajifunze zaidi juu ya ubunifu na kuongeza ubora kwenye kazi zao, wakirudi tunaamini wataweza kuwafundisha vijana wengi zaidi, na kutimiza lengo letu la kuwasaidia vijana kujiajiri’ alimaliza Mwita.
Toa Maoni Yako:
0 comments: