NA VERONICA KAZIMOTO, KAMPALA.

WITO umetolewa kwa washiriki wote wa Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika kuelendelea kutoa takwimu sahihi na kwa wakati ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.

Wito huo umetolewa jana na Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ruhakana Rugunda wakati akifungua Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Speke Munyoyo Kampala, Uganda.

Dkt. Rugunda amesema kuwa, ili kupata maendeleo kwa haraka, ni lazima takwimu zitolewe kwa wakati na ziwe sahihi kwa ajili ya kusaidia kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

"Ili Bara la Afrika liweze kuendelea kwa haraka, linahitaji takwimu sahihi na zinazotolewa kwa wakati ili takwimu hizo zisaidie katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo", amesema Waziri Mkuu Rugunda.

Dkt. Rugunda ameongeza kuwa ili kuweza kufanikisha hilo, kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kusaidia program mbalimbali za uzalishaji wa takwimu na matumizi yake kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.

Kwa upande wa Waziri wa Fedha wa Uganda Matia Kasaija amesema kuwa, ili kuweza kulinganisha takwimu za nchi mbalimbali, ni vyema takwimu zinazozalishwa zikafuata mbinu bora za uzalishaji wa takwimu.

Matia Kasaija amesema mbinu bora za uzalishaji wa takwimu ni zile zinazofuata viwango vinavyopendekezwa na Umoja wa Kimataifa - Kitengo cha Takwimu.

Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika umewakutanisha washiriki takribani 400 kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania. Mkutano huu ni wa siku tatu na unatarajia kumalizika kesho tarehe 15 Januari, 2015.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: